Watuhumiwa mishahara hewa wafikishwe kortini

04Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Watuhumiwa mishahara hewa wafikishwe kortini

UTEKELEZAJI wa mkakati wa Serikali katika kudhibiti malipo hewa ya mishahara kwa watumishi hewa wa umma unaendelea kushika kasi.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ni kwamba hadi sasa kazi ya uhakiki kwa nia ya kuwatambua watumishi hewa iko katika hatua nzuri, lengo likiwa ni kukomesha upotevu wa mabilioni ya fedha yaliyokuwa yakilipwa kila mwezi kupitia hujuma hiyo.

Matarajio ni kuona kuwa fedha hizo zitakazookolewa kupitia operesheni kabambe ya kubaini undani wa wizi uliokuwa ukifanyika zitaelekezwa katika maeneo mengine ya maendeleo yanayowagusa moja kwa moja wananchi wa kawaida, ikiwamo kuboresha huduma za afya, elimu, maji na miundombinu.

Aidha, kupitia operesheni hiyo, wahusika wote wanatarajiwa kuchukuliwa hatua stahili za kisheria.

Taarifa iliyoripotiwa jana na gazeti hili ilimkariri Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma akisema kuwa hadi sasa, kuna watu zaidi ya 500 wanatuhumiwa kuwamo katika mtandao uliokuwa ukijinufaisha kupitia mishahara hewa.

Ilielezwa zaidi kuwa uchunguzi mkali kupitia vyombo mbalimbali vya dola, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ungali ukiendelea na kwamba, hatua zitakazofuata ni kuwafikisha mahakamani wahusika wote wa kashfa hiyo.

Aidha, kadri uchunguzi utakavyoonyesha, baadhi ya watuhumiwa watachukuliwa hatua za kinidhamu kulingana na sheria za utumishi wa umma.

Sisi tunapongeza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kuhusiana na hujuma hizo za fedha za umma. Tunaunga mkono harakati hizo zilizoshika kasi zaidi baada ya kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya tano ya Rais John Magufuli kutokana na ukweli kwamba vitendo hivyo, siyo tu vimekuwa vikidhoofisha jitihada za maendeleo, lakini pia wizi wa aina hiyo umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa kushusha ari ya kujituma kwa watumishi wema wanaotambua kuwa wenzao hujitajirisha kupitia njia hiyo haramu.

Kwa mfano, inafahamika wazi kuwa mara zote, Serikali imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha kuwa inaboresha huduma za kijamii kupitia miradi mbalimbali ya barabara, maji, elimu na afya. Hata hivyo, ukosefu wa fedha kukidhi mahitaji ni changamoto mojawapo kubwa kwa taifa.

Katika taarifa ya Serikali ya hivi karibuni, ilielezwa kuwa kiasi cha takribani Sh. bilioni 16.4 kimekuwa kikipotea kila mwezi kutokana na malipo ya mishahara kwa watumishi hewa. Kwa hesabu rahisi, ni kwamba walau Sh. bilioni 196.8 zimekuwa zikiishia mifukoni mwa watu wachache kwa mwaka. Kiasi hicho ni kikubwa, hasa kwa kuzingatia kuwa kwa wastani, gharama za uchimbaji wa kisima cha maji safi na salama huwa si zaidi ya Sh. milioni 50; hivyo, walau visima 3,936 vingeweza kuchimbwa nchini kote kila mwaka endapo fedha hizo zingeelekezwa katika miradi ya maji.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndipo tunapoona kwamba jitihada za kukomesha ulipaji wa mishahara hewa zinapaswa kuungwa mkono na kila mmoja. Lililo muhimu pia ni kuhakikisha kwamba watuhumiwa wote wanafikishwa mahakamani mara tu uchunguzi unapokamilika ili mwishowe waipate haki yao.

Kwamba, wale watakaothibitika kujihusisha na mtandao wa mishahara hewa wahukumiwe kulingana na sheria za nchi huku wasio na hatia wawe huru kulitumikia taifa.

Shime, vyombo vya uchunguzi kuhusiana na kashfa ya mishahara hewa viendelee kufanya kazi yake kwa umakini ili watuhumiwa wote wafikishwe mahakamani.

Habari Kubwa