Watumishi waitendee haki mishahara mipya

07Nov 2017
Mhariri
Nipashe
Watumishi waitendee haki mishahara mipya

Hatimaye serikali ilitangaza kuwaongezea mishahara watumishi wa umma nchini na pia kuwapandisha madaraja wale wanaostahili kuanzia mwezi huu.

Neema hiyo kwa watumishi wa umma ilitangazwa rasmi na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, wakati akielezea mafanikio ya miaka miwili tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano.

Katika taarifa hiyo, Serikali ilieleza vilevile kuwa mbali na kuongeza mishahara na kuwapandisha madaraja watumishi wake, pia italipa stahiki zote kwa wanaostahili.

Hakika, hiyo ni habari njema. Ni neema kubwa. Ni taarifa ambayo kwa namna yoyote ile, inatarajiwa kuwapa faraja ya kipee watumishi wengi wa umma.

Furaha ya kupokea mishahara mipya iliyoboreshwa kuanzia mwezi huu, kupandishwa madaraja na pia kulipwa stahiki zao inatarajiwa kuongezwa na ukweli kwamba kwa muda mrefu sasa, jambo hilo halikuwahi kufanyika.

Tangu Machi mwaka jana, Serikali ilisitisha upandishaji mishahara na madaraja kwa watumishi wa umma ili kupisha kazi ya uhakiki wa idadi kamili ya watumishi wake na pia kuwabaini wale wote wenye vyeti bandia vya kielimu.

Watumishi zaidi ya 10,000 walighundulika kuwa na vyeti feki huku wengine takribani 20,000 wakigundulika kuwa ni watumishi hewa, hivyo kwa ujumla serikali kuokoa zaidi ya Sh. bilioni 300 ambazo sasa zinaweza kutumika kwa shughuli nyingine za maendeleo.

Sisi tunaipongeza serikali kwa hatua yake hii, hasa kwa kutambua kuwa athari chanya za malipo mazuri kwa watumishi wa umma huwanufaisha siyo wao na familia zao tu, bali na wananchi wengine kwa ujumla. Na hili lipo wazi.

Watumishi wa umma wanapolipwa vizuri, maana yake na wao watakuwa na nguvu zaidi ya kulipia mahitaji mbalimbali ya bidhaa na huduma. Kufanya hivyo huongeza kasi ya mzunguko wa fedha na mwishowe kuwanufaisha Watanzania wengi zaidi.

Jambo pekee tunaloamini kwamba linapaswa kuzingatiwa na wanufaika wa nyongeza hiyo ya mishahara kwa watumishi, ni kuboreshwa zaidi kwa huduma.

Sisi, tunaamini kuwa furaha ya mishahara mipya kwa watumishi itaendana na huduma bora zaidi kwa wananchi kulinganisha na vile ilivyokuwa hapo kabla.

Kwa mfano, hatutarajii kuona kuwa walimu wakiwa watoro kwenye vituo vyao vya kazi bali kuwajibika zaidi na kuhakikisha kuwa malengo ya elimu yanatimia.

Hatutarajii pia kuona kuwa madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa afya wakilalamikiwa kwa uzembe bali kusifiwa na wananchi kutokana na uchapakazi bora unaotokana na kujituma kazini kila uchao.

Aidha, vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo ni kinyume cha sheria ya nchi na vimekuwa vikipigwa vita kwa kasi kubwa zaidi tangu serikali ya awamu tano iingie madarakani, kamwe havitapata nafasi kuanzia mwezi huu. Kwa ujumla, ni imani yetu kwamba madaraja mapya na mishahara mipya kwa watumishi vinapaswa kuwa chachu ya kuimarika kwa huduma katika idara, taasisi na mashirika ya umma.

Hakika, hilo ndilo kusudio la serikali katika kutimiza wajibu wake huo kama mwajiri, ikitaraji kuwa tija itaongezeka katika mahala pa kazi. Siyo kinyume chake.

Ni imani yetu kwamba sasa, hakuna mtumishi wa umma atakayebweteka kwa furaha. Badala yake, kila mmoja atatekeleza wajibu wake kadri inavyotakiwa ili.

Kufanya hivyo kutaiwezesha serikali kutimiza malengo yake katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

Watumishi wa umma waitendee haki nyongeza hiyo ya mishahara, madaraja na kulipwa kwa stahili zao kuanzia mwezi huu.

Wanufaika wasiiangushe serikali kwa kuendelea kufanya kazi kwa mazoea bali sasa wafanye kazi kwa kujituma zaidi ili kuinua tija kwenye maeneo yao na mwishowe kuwanufaisha Watanzania.

Habari Kubwa