Wauguzi waendelee kuzingatia maadili

14May 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wauguzi waendelee kuzingatia maadili

WAUGUZI ni miongoni mwa wafanyakazi muhimu wanaotegemewa katika sekta ya afya, Mei 12, wameungana na wenzao kuadhimisha ya siku ya Uuguzi na Ukunga Duniani.

Mwaka huu kitaifa maadhimisho hayo yamefanyika mkoani Katavi kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi Sauti inayoongoza Afya kwa Wote.

Katika maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuudhuriwa na wauguzi na wakunga wa MNH na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambapo walikumbushwa mambo kadhaa.

Pamoja na mambo mengine wametakiwa kuendelea kutekeleza majukumu ya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kitaaluma kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa.

Wito huo ulitolewa na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Agnes Mtawa, aliwakumbusha wauguzi kuzingatia mafunzo yanayotolewa mahala pa kazi kwani ndio yanayochochea kutoa huduma bora ya afya kwa wagonjwa.

Aliwataka wauguzi kutambua kwamba huduma wanayotoa kwa wagonjwa ni ya kibinadamu, pia aliwatia moyo kuwa hivi sasa malalamiko mengi yamepungua.

Tunaunga mkono pongezi hizo, hata hivyo tunawataka wasibweteke wakawa kama mgema kwa kusifiwa tembo akalitia maji, tunatamani kuona kwamba wagonjwa wanapata huduma bora zinazowasaidia kuokoa maisha yao.

Tunaelewa kuwa kuna malalamiko ya msingi na mengine yanachangiwa na mazingira, lakini ukweli unabaki kuwa mgonjwa anahitaji huduma bora. Wapo wauguzi wenye maneno makali ambayo huwafanya wagonjwa kuzidiwa, kwa kifupi tumeshuhudia malalamiko mengi hadi kutoka kwa wajawazito wanapokwenda kujifungua, wapo wauguzi kadhaa ambao wamechukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya.

Miongoni mwa makosa hayo ni pamoja na kuwatelekeza wajawazito wakiwa kwenye hatua ya kujifungua, wapo wanaodaiwa kusababisha vifo kutokana na huduma mbovu kwa wagonjwa.

Pia wapo wauguzi ambao wamepata tuzo za aina mbalimbali kutokana na kuzingatia maadili ya kazi zao na kufanya kazi kwa kujituma.

Pamoja na kwamba kuna wakati mnaweza kukumbana na wakati mgumu kutokana na sababu mbalimbali, bado mnawajibika kutumia lugha nyepesi kuwaelewesha wagonjwa ili waelewe badala ya kuwafokea.

Tunatambua wauguzi ni wanataaluma, hivyo wana mafunzo maalum ambayo wamepewa ili kutoa huduma bora kwa wagonjwa, ni vyema wakizingatia ikiwa ni pamoja na kujitahidi kuwa wavumilivu hata wanapokutana na wagonjwa machachari wajue jinsi ya kuwahudumia.

Ni vyema wanapokutana na udhalilishaji wa aina yoyote wajitahidi kuhakikisha wanaushughulikia jinsi inavyotakiwa, siyo vyema kubeba chuki na kuihamishia kwa wagonjwa wengine.

Kazi ya uuguzi na ukunga licha na kuwa ni ya wito, lakini pia inahitaji kuwa na hofu ya Mungu, ili kumudu kujituma kuokoa maisha ya wagonjwa kwa kuwapa huduma inayostahili kwa mujibu wa maelekezo ya mafunzo mliyopata.

Huwezi kuzungumzia huduma bora ya tiba kwa mgonjwa pasipo kuhusisha pembe tatu, ambazo ni madaktari, wauguzi pamoja na vifaa tiba na dawa.

Tunawasisitiza wauguzi watambue umuhimu wao katika huduma ya afya, ni wazi kwamba madaktari wataelemewa iwapo wauguzi hawatakuwapo kwenye sekta hii hii ya huduma ya afya, hivyo jamii inawategemea katika kupata tiba bora.

Habari Kubwa