Wauzaji mbegu dumavu vifaranga vya kuku washughulikiwe

23Sep 2022
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wauzaji mbegu dumavu vifaranga vya kuku washughulikiwe

HABARI kuhusu wafugaji wa kuku kulia kwa kuuziwa vifaranga vilivyodumaa, hazifurahishi na inaua soko la kuku nchini.

Hivi karibuni kulikuwa na kilio cha upungufu wa kuku katika masoko mengi jijini Dar es Salaam, na sababu ikielezwa kuwa kumekuwa na upungufu mkubwa wa soko la vifaranga.

Baadhi ya wafanyabiashara kwenye sekta hiyo wanatumia mwanya huo kuwauzia wafugaji vifaranga ambavyo ni dumavu na kuingia hasara kubwa kutokana na kutumia muda mrefu kuvikuza na gharama ya chakula.

Vifaranga vya kuku vinavyolalamikiwa ni vya kuku wa nyama ambao wana soko kubwa nchini, hasa jijini Dar es Salaam.

Ukiangalia katika migahawa, wauza chips, wanaojishughulisha na upishi wa vyakula kwenye sherehe na hotelini kuku wa nyama ni bidhaa muhimu na pengine ndiyo kitoweo rahisi kukipata.

Inapotokea bidhaa hiyo kuadimika inaathiri sio wafugaji pekee bali hata wafanyabiashara wa sekta tajwa.

Baadhi ya wafugaji wanalalamika kuwa wamekuwa wakipata hasara na kukatishwa tamaa ya kuendelea na biashara hiyo kutokana na udanganyifu unaofanywa na watu wachache wanaojipatia pesa kwa njia isiyo halali.

Wafugaji hao wanachosema ni kuwa wanapouziwa vifaranga hivyo ni vigumu kubaini kama ni dumavu mpaka muda wa kuuza unapowadia, ndipo hubaini kuwa havikui kama ilivyo kawaida kwa vifaranga walivyozoea kuvinunua.

Hali hii haiwaumizi wafugaji pekee bali hata walaji wa kitoweo hicho, kwani wamekuwa wakilalamika kuku wanaouziwa ni wadogo kama ndege.

Kwa kweli soko hili la kuku linapohujumiwa, linaathiri watu wengi ambao hutegemea vipato vyao kupitia ufugaji wa kuku.

Ukiangalia wajasiriamali wengi wanaoanza kufanya biashara huanzia kwenye ufugaji kuku na wengi wao ni kinamama.

Ufugaji kuku umewasaidia kuendeleza familia zao kwa kuwasomesha watoto, kuzalisha biashara nyingine na kujenga nyumba bora na za kisasa.

Ukosefu wa ajira nchini, kwa kiasi fulani umepata ufumbuzi kwa watu kujiajiri wenyewe kupitia ufugaji, ukiwamo wa kuku.

Kwa hiyo sekta hiyo inapohujumiwa kweli inaathiri watu wengi sana na wanapokosa shughuli nyingine ya kufanya serikali pia inaathirika.

Kutokana na kilio hicho, tunashukuru serikali imekisikia na kuahidi kufuatilia kwa kuchukua hatua kwa wote wanaohusika na udanganyifu huo.

Pia serikali imekiri kuna mbegu dumavu za vifaranga mbavyo havikui kwa wakati. Hata hivyo imefafanua kuwa wakati mwingine ni matunzo na chakula cha mfugaji mwenyewe kinaweza kusababisha kuku wasikue kwa wakati.

Ufafanuzi huo ni sahihi kabisa, lakini kuna haja ya kutolewa kwa elimu itakayowaelewesha wafugaji kutambua kipi chakula kinachofaa na kipi kisicho faa kwa sababu wengine hawana elimu hiyo.

Na pia kuna baadhi ya watu wanaotumia fursa ya ufugaji kwa kutambua kuwa kuna mahitaji mengi ya chakula cha kuku, kujitengenezea kienyeji na kuathiri wafugaji.

Ufugaji kuku ni fursa mtambuka ambayo inagusa kila eneo, kitoweo hicho kinahitajika kwa matumizi ya nyumbani na kwa biashara. Wapo wanaojiajiri kwa kutegemea kuuza miguu ya kuku, vichwa, utumbo. Kama kuku huyo hatakuwa kwa kiwango kinachotakiwa hata hiyo biashara haiwezi kuwa na uhitaji unaotakiwa.

Wanaohujumu ufugaji wa kuku lazima washughulikiwe ili wasiendelee kuathiri maisha ya wengine.

Habari Kubwa