Wawakilishi wa Tanzania Caf sajilini kwa umakini

10Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wawakilishi wa Tanzania Caf sajilini kwa umakini

KWA mara ya kwanza katika soka la Tanzania, katika msimu mpya wa 2019/2020, Tanzania Bara itawakilishwa na timu nne kwenye michuano ya kimataifa, mbili Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho Afrika.

Tayari Shirikisho la Soka Afrika (Caf), limethibitisha kuwapo kwa nafasi hizo na kulitaka Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuhakikisha hadi mwishoni mwa mwezi huu linasajili timu zake zitakazoshiriki mashindano hayo kupitia mtandoa (CMS).

Na kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu zilizofanyiwa marekebisho na Kamati ya Utendaji ya TFF baada ya kupatikana nafasi hizo nne, timu zitakazoiwakilisha Tanzania Bara ni Simba na Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa, huku Azam FC na KMC zikipeperusha bendera ya nchi katika Kombe la Shirikisho.

Ikumbukwe kupatikana kwa nafasi hizo nne kutoka mbili za awali, kumetokana na mafanikio makubwa ya Klabu ya Simba baada ya kufanikiwa kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kabla ya kutolewa na TP Mazembe katika msimu huu uliomalizika wa 2018/19.

Kufika kwa Simba katika hatua hiyo kuliiwezesha Tanzania Bara kuvuna pointi 15, hivyo ukichanganya na pointi tatu ambazo zilipatikana kwa kipindi cha misimu mitatu iliyopita wakati Yanga ikishiriki michuano hiyo, ilifanya Tanzania kuwa na jumla ya pointi 18.

Kwa mantiki hiyo, Tanzania Bara ikafanikiwa kuwa timu ya 12 kwa ubora, huku ikizipita Ivory Coast (pointi 15) na Kenya (pointi 14) iliyokuwa ikitegemea mafanikio ya Gor Mahia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ambayo nayo iliishia hatua ya robo fainali.

Aidha, ikumbukwe pia nafasi hizo nne si za kudumu, kwani ikitokea katika michuano ya msimu ujao wa 2019/20 nchi nyingine klabu yake/zake zikafanya vizuri na kuvuna pointi zaidi, moja kwa moja Tanzania Bara itapoteza nafasi hizo na kurejea kwenye mbili za awali.

Pointi hizo hutolewa kadri klabu za nchi shiriki kwenye michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu Afrika, zinavyofanya vizuri kwa kusonga mbele.

Kinachotakiwa sasa ni Simba, Yanga, Azam FC na KMC kuhakikisha zinajipanga vizuri kuelekea michuano hiyo ili kuweza kuongeza pointi zaidi ili Tanzania Bara iendelee kupata nafasi hizo nne.

Na katika hilo, Nipashe tunaishukuru Caf kwa kuijulisha TFF mapema kuongezeka kwa nafasi hizo kwani kunatoa nafasi chanya kwa klabu kujiandaa mapema hususan kipindi hiki cha dirisha la usajili.

Kinachotakiwa kwa wawakilishi wetu hao ni kuhakikisha wanafanya usajili makini kulingana na mashindano hayo ya kimataifa yaliyopo mbele yao na si vinginevyo.

Hatutarajii kuona moja ya wawakilishi wetu katika michuano hiyo akifanya usajili kwa kuita wachezaji kwa ajili ya majaribio kwanza, bali usajili unaotakiwa ni wa nyota ambao tayari walishawachunguza wakicheza na waliokidhi viwango kulingana na mapendekezo ya makocha.

Lengo na matarajio yetu ni kuona wawakilishi wetu wote kwanza wanafika hatua ya makundi na kisha robo fainali na hatimaye nusu na  kucheza fainali.

Hilo likifanikiwa hakika Tanzania Bara itakuwa imejiongezea pointi na kuwa na uhakika wa kuingizia timu nne msimu unaofuata wa 2020/2021, kwani pointi nyingi huanza kutolewa katika hatua hizo.

Tunaamini hilo linawezekana kama maandalizi yataanza sasa kwa kusajili wachezaji wenye viwango vya hali ya juu, lakini pia wazoefu wa mechi za kimataifa, huku uboreshwaji wa mabenchi ya ufundi ya klabu hizo ukizingatiwa pia. Kila la Kheri Simba, Yanga, Azam na KMC katika dirisha la usajili.

Habari Kubwa