Wawakilishi wetu michuano CAF msilale bado dakika 90

13Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wawakilishi wetu michuano CAF msilale bado dakika 90

wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa walioanzia hatua ya awali, Yanga, Azam FC na Biashara United, tayari wamemaliza dakika 90 za kwanza na kilichobaki ni muda mwingine kama huo zitakaporudiana mwishoni mwa wiki hii.

Katika michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Yanga na Simba zinaiwakilisha Tanzania Bara kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini 'Wekundu wa Msimbazi' hao wao wanaanzia moja kwa moja kwenye raundi ya kwanza.

Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC na Biashara United ndizo zinazobeba jukumu hilo la kuhakikisha bendera ya Tanzania inapepea vema kimataifa katika michuano hiyo ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu Afrika baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa.

Ukiacha matokeo ya jana kati ya Yanga na Rivers United ya Nigeria ambayo hadi gazeti hili linakwenda mitambo timu hizo zilikuwa bado hazijafungana kwenye mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, upande wa pili Azam FC na Biashara United zimeanza vema kinyang'anyiro hicho.

Biashara United ambayo ilianzia ugenini dhidi ya Dikhil ya Djibouti, iliibuka na ushindi wa bao 1-0 wakati Azam FC nayo ilipata ushindi mnono nyumbani katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam baada ya kuichapa Horseed ya Somalia mabao 3-1.

Kwa ujumla ni matokeo mazuri kwa wawakilishi wetu hao, lakini hawapaswi kubweteka na kusahau kujipanga vema kuelekea mechi za marudiano mwishoni mwa jumla kwa kuwa hizo ni dakika 90 za kwanza bado zingine kama hizo na lolote linaweza kutokea kwenye mechi za marudiano kwa wapinzani wao kupindua meza.

Kwa Yanga yenyewe itakuwa ugenini nchini Nigeria, hivyo inapaswa kufanya maandalizi makubwa zaidi na kujipanga kwa kila kitu ndani na nje ya uwanja hususan kuwaandaa wachezaji kisaikolojia kwa kila kitakachotokea.

Lakini kwa Azam FC kama ilivyo kwa Biashara United, zenyewe zitakuwa nyumbani katika mechi hizo za marudiano, lakini hilo haliwezi kuwa sababu ya kuacha kujiandaa vema kwani mara nyingine mpira una matokeo ya ajabu na wapinzani wao wanaweza kupata matokeo chanya na kuwatoa.

Tunaamini kama Biashara United ilishinda ugenini, pia Dikhil inaweza kujipanga na kupata ushindi kwenye mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, hivyo kikubwa wawakilishi hao wa Tanzania wote kwa ujumla hawapaswi kuwadharau wapinzani wao na badala yake wanatakiwa kufanya maandalizi makubwa zaidi.

Kwa Azam FC ambayo imepata bahati ya mechi zote mbili kuchezwa hapa nchini kutokana na hali ya usalama Somalia kutokuwa shwari, bado hawapaswi kubweteka na kusahau kujipanga vizuri kwani lolote linaweza kutokea na Wasomali hao kupata matokeo chanya yatakaowawezesha kusonga mbele.

Aidha, pamoja na mashabiki kutoruhusiwa kuhudhuria mechi hizo kutokana na janga la ugonjwa wa COVID-19 linaloitesa dunia, wachezaji na makocha hawana budi kutambua wadau wa soka nchini na Watanzania kwa ujumla wapo nyuma yao kwa kila aina ya sapoti wakitaka matokeo chanya.

Lengo letu ni kuona wawakilishi wote wanasonga mbele na kutinga hatua ya makundi ili kulinda nafasi ya Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano hiyo ya CAF kila mwaka, na hilo linawezekana tu kama wawakilishi wetu kila mechi wataichukulia kama fainali. Hivyo, tunawatakia maandalizi mema kuelekea mechi hizo za marudiano kimataifa.