Wazalishaji dawa wazalishe zaidi, punguzo VAT lifuate

01Nov 2017
Mhariri
Nipashe
Wazalishaji dawa wazalishe zaidi, punguzo VAT lifuate

MOJA ya changamoto ambazo Serikali imezifanyia kazi na kuleta matokeo chaya ni ya upatikanaji dawa katika vituo vya huduma vikiwamo zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, rufani na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Uhaba wa dawa katika vituo vya umma kabla ya Serikali ya Rais John Magufuli kuingia madarakani ulikuwa mkubwa kiasi kwamba wagonjwa walikuwa wanakosa dawa na vifaa tiba na kuelekezwa kwenda kununua maduka binafsi.

Changamoto hiyo iliifanya serikali kuchukua hatua, na miongoni mwa hatua hizo ni kuruhusu vituo vya huduma kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji badala ya kuviachia kuagiza kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Utaratibu wa vituo kuagiza dawa kupitia MSD ulikuwa unasababisha dawa kuchelewa kufika kutokana na MSD kuelemewa, hivyo kusababisha athari kwa wagonjwa.

Mbali na MSD kukabiliwa na changamoto ya kusambaza dawa vituo vyote nchini, pia ilikabiliwa na changamoto ya kudaiwa na wazalishaji kutokana na kuidai Serikali muda mrefu, hivyo kukosa uwezo wa kuagiza dawa kutoka kwa wazalishaji.

Hatua iliyofuata ni serikali kuanza kulipa ,madeni ya MSD, hivyo kuipa uwezo wa kuendelea kukunua na kuagiza dawa kutoka kwa wazalishaji nje na ndani ya nchi.

Serikali imeshaweka wazi kwamba sasa upatikanaji wa dawa ni wa kuridhisha kwa kiwango kikubwa katika vituo vyote vya huduma nchini.

Hivi karibuni shirika lililo la kiserikali ambalo limekuwa likifuatilia masuala ya afya ikiwamo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwenye vituo vya huduma nchini la Sikika, lilisema kuwa utafiti wake katika wilaya takribani 20 nchini umebaini upatikanaji wa dawa umeongezeka kwa asilimia 30 katika takribani kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Wakati serikali ikiendelea na hatua za kuhakikisha upatikanaji wa dawa unaongezeka, wazalishaji wa dawa wameomba kupunguziwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kuwarahisishia uzalishaji. Ombi hilo liliwasilishwa kwa Rais Magufuli jana jijini Mwanza wakati wa uzinduzi wa Kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu kilichopo eneo la Buhongwa.

Akijibu ombi hilo, Rais Magufuli alisema kwa sasa serikali haiwezi kuwapunguzia VAT kwa kuwa uzalishaji wa dawa bado ni mdogo kulinganisha na mahitaji makubwa ya dawa.

Hata hivyo, alisema upo uwezekano wa kulijadili ombi hilo kwa kuwa mawaziri wake walikuwapo jana, lakini alisisitiza kwamba suala la msingi katika kufikia makubaliano ya punguzo hilo la kodi ni kwa wazalishaji kuongeza uzalishaji na pia kuzalisha dawa bora zinazokidhi viwango.

Wazalishaji wa dawa wa ndani wana uhakika wa kupata soko la bidhaa hiyo kutokana na mahitaji makubwa kwenye vituo vingi vya huduma vilivyoko nchini. Tunakubaliana na kauli ya Rais Magufuli ya kuwataka wazalishaji hao kwanza kuonyesha umakini katika suala zima la kuzalisha dawa za kutosha na zenye ubora unaokidhi viwango.

Changamoto aliyowapa pamoja na malengo mengine, itasaidia na kupunguza uagizaji wa dawa kutoka nje, ambazo gharama yake ni kubwa zaidi na wakati mwingine inachukua muda mrefu kufika.

Wanachotakiwa kufanya wazalishaji wa dawa nchini ni kuchangamkia fursa ya kuzalisha dawa zaidi na zenye ubora unaokidhi viwango. Baada ya hapo, itakuwa rahisi kwa serikali kutathmini kama iwapunguzie kodi hiyo ama la.

Tumefika wakati sasa taasisi na watu binafsi wanapokutana na viongozi wakuu wa serikali kama Rais, Makamu na Waziri Mkuu wasitangulize kuomba misamaha au kupunguziwa kodi, bali wawadhihirishie kwa vitendo mafanikio yao. Kama kutakuwa na changamoto zinazowakwaza, maombi kama hayo yafuate.

Habari Kubwa