Wazazi na walezi tuacheni mila zinazokwamisha elimu

29Sep 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wazazi na walezi tuacheni mila zinazokwamisha elimu

ILI mabinti wa Tanzania wapate elimu bora kuna kila sababu ya wazazi na walezi kuachana na tamaduni na mila zinazowaponza hasa kuwaachia watoto kuingia kwenye mafundisho na taratibu ambazo zinawaelekeza kufanya ngono wakiwa kwenye umri mdogo.

Tamaduni hizo ni pamoja kuwacheza mabinti ngoma wanapokaribia kupevuka au kufikia umri wa balehe na haya ni mambo yanayofanyika baada ya wanafunzi kumaliza darasa la saba.

Mwaka huu mtihani huo ambao umesogezwa mbele kutokana na shule kufungwa miezi mitatu ili kuepusha maambukizi ya COVID-19 unatarajiwa kufanyika kuanzia wiki ijayo.

Mabadiliko na kuachana na mila hizo ni jambo la msingi kwa sababu mabinti hao ni wadogo na wengi bado wako shuleni na wanatarajiwa kusoma zaidi hadi sekondari na kufikia vyuo vikuu. Ikumbukwe kuwa serikali inawekeza katika elimu na ndiyo inayogharamia elimu msingi kuanzia msingi hadi sekondari.

Tunashauri kuwa ni vyema jamii ikajielewa na kukubaliana nasisi kwamba kuwacheza watoto wa kike ngoma wakiwa masomoni kunawaathiri kisaikolojia na kusababishwa kushindwa kuendelea na masomo.

Tunaona kuwa ngoma na mafundisho yanayojielekeza kwenye masuala ya ngono ni vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya elimu katika mikoa na jamii zinazoendelea kuenzi mila na desturi zisizo na tija wala ustawi wa taifa.

Tunawahimiza na kuwataka wazazi na walezi kuachana na mila hizo potofu za kuwacheza ngoma watoto wa kike wakiwa bado wanasoma shule kwani wanawaharibu kisaikolojia, kimaadili na hasa katika masomo yao.

Tunaamini kuwa mtoto wa kike anapochezwa ngoma anapohitimu darasa la saba kuanzia mwezi ujao hakumsaidii kwa vile wengi wanakuwa wameandaliwa na kuwekwa tayari kuolewa au kujiingiza kwenye masuala ya ndoa.

Tunawashauri wazazi, walezi na walimu kushirikiana kwani inawezekana wengi hawajafahamu kuwa kufanya hivyo ni kuwandaa kuwa wali wanaosubiri kuolewa?

Aidha, sote tufahamu kuwa ni jukumu letu kusisitiza kuwa ili watoto wa kike wasome kuna kila sababu kama taifa kufanya jitihada za kuwapeleka kwenye njia zilizonyooka badala ya kuwaingiza kwenye mitego.

Lakini pia, tunawashauri viongozi hasa wale wanazungukwa na mila za kuwacheza mabinti ngoma na kuwaingiza kwenye mahusiano wakiwa wadogo, kuona namna ya kupeleka mapendekezo ya kutunga sheria ndogo ndogo zitakazopiga marufuku mabinti wanaosoma kuchezwa ngoma.

Tunayasema haya kwa sababu baadhi ya wazazi na walezi wanasubiri mtihani wa darasa la saba kumalizika ili kuandaa sherehe hizo za ngoma za unyago.

Tunaamini wakati umefika kwa watendaji kata, maofisa elimu kata, kamati za elimu na uongozi wa vijiji kulisimamia hilo na kuwashauri wazazi na walezi kusubiri hadi hapo wasichana watakapomaliza masomo.

Tunawakumbusha kuwacheza ngoma watoto ni moja ya sababu inayoshusha ufaulu wa wanafunzi katika mikoa inayoendekeza utamaduni ukiwamo huo wa unyago.

Ni wakati wa kuona kuwa tunawasaidia wasichana kufaulu kwenda shuleni, kuingia darasani na kusoma pamoja kufundishwa ipasavyo.

Lakini sisi wazazi na walezi kusimamia nidhamu ya watoto wetu nyumbani na ndani ya jamii na kuwa karibu nao katika kuwashauri umuhimu wa elimu na kujua namna ya kujitegemea na kuendesha maisha yao sasa.

Tusiiangushe serikali wakati ikitekeleza majukumu yake kwa kuhakikisha kunakuwapo na walimu, miundombinu, vitabu, maabara na kugharamia mahitaji mengine kulingana na kile shule inachohitaji.

Tunawakumbusha wazazi na walezi kuachana na tamaduni ambazo zinakuwa kikwazo kwa watoto kusoma. Tuwalinde watoto wetu wanaomaliza shule wiki ijayo na tuweke utaratibu unaozielekeza shughuli hizo kufanyika baada ya watoto kufikia umri wa kujitambua na kujua mambo mema na mabaya.

Habari Kubwa