WB, serikali zina nafasi kuondoa umaskini huu

06Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
WB, serikali zina nafasi kuondoa umaskini huu

LICHA ya jitihada nyingi kufanyika kuondoa umaskini, wadau wa maendeleo wakiwamo Benki ya Dunia (WB) wanaeleza kuwa umaskini ni changamoto nchini na kwamba idadi ya watu hao inaongezeka.

Ripoti ya chombo hicho cha fedha duniani inayotolewa wiki hii jijini Dar es Salaam, inasema kuwa maskini wameongezeka kutoka milioni 12.3 mwaka 2012 hadi kufikia milioni 14 mwaka jana.

Si habari njema lakini ni jambo linalolipa taifa changamoto ya kujitahidi zaidi kuondoa umaskini ambao kwa miaka mingi ni maradhi yanayolitesa taifa tangu uhuru mwaka 1961 hadi leo takribani miaka 58.

Pamoja na taarifa hiyo , ukweli ni kwamba serikali imeweka mipango na mikakati kadhaa ya kuondoa umaskini ili kila Mtanzania aweze kumudu maisha yake ikiwa ni pamoja na kuweka mikopo ya kinamama, vijana na watu wenye ulemavu.

Kwa mfano, inawasomesha watoto wote bure kuanzia elimumsingi inayojumuisha pia sekondari.

Aidha, imeanzisha mfumo wa kutumia mfuko maalumu kuzisaidia kaya masikini kwa kuzipatia ruzuku na huduma nyingine kazi inayofanywa kupitia Mfuko wa Taifa wa Maeneleo ya Jamii (Tasaf).

Lakini, si hivyo tu, kuna mpango wa kuwasaidia watu wenye ulemavu na mahitaji maalumu kusoma. Katika mchakato huo wa kusoma hadi kufika chuo kikuu serikali imeeleza kuwa wapo watakaosamehewa kulipa mikopo waliyopewa ili kuwapunguzia mzigo wa kulipa madeni. Nia ni kuendelea kuwawezesha kwa kila namna ili wamudu maisha yao.

Mambo mengi yanayofanywa hayamaanishi kuwa umaskini utaondoka kwa siku moja. Ni mchakato unaohitaji ushirikishwaji na ushirikiano baina ya wadau hao wa maendeleo na serikali.

Mikakati ya kuondoa umaskini inahusisha kujenga uchumi ikiwamo miundombinu, viwanda na miradi mingine mingi kama kuendeleza kilimo na ufugaji , uchimbaji madini na kuongezea thamani bidhaa zinazozalishwa nchini.

Pamoja na kusikia ripoti ya Benki ya Dunia ni wakati pia wa wadau hao wa maendeleo kuongeza mchango wao kusaidia kupunguza umaskini kwa kufanikisha juhudi za kuanzisha viwanda vya kusindika mazao na kuzalisha bidhaa zilizoongezewa thamani vijijini waliko Watanzania wengi.

Kwa kuliona hilo tunaoimba WB kusaidia utafiti unaowezesha kupatikana teknolojia rahisi na za gharama nafuu ili kutumiwa kuondoa umaskini vijijini.

Teknolojia hizo tunaamini zitafanikisha uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa mazao vijijini ambako suala la kujenga vihenge vya kutunza chakula kwa utaalamu ni tatizo linalozikabili jamii nyingi.

Ni wazi kuwa WB ina mchango kwenye maendeleo ya nchi, tunajua kuwa ina nafasi ya kushirikiana zaidi na serikali kwenye kuwatambua watu maskini zaidi walioko sehemu mbalimbali na kushirikiana na serikali kufanya utafiti wa kuibua mikakati ili waondokane na umaskini huo.

Tunaona kuwa ni wakati wa kuibua mikakati ya kuwekeza zaidi vijijini na kuboresha maisha ya sehemu hizo ili kupunguza idadi ya watu wanaokimbilia mijini kwa kuwa vijijini au mashambani kuna maisha duni.

Hapo ndipo tunapoishauri WB na serikali kuona uwezekano wa kuwa na vyuo vya ufundi maalumu kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali ya watu wanaoishi vijijini ili waweze kumudu maisha yao na kupunguza umaskini.

Vyuo hivyo vinaweza kuanzishwa baada ya kutambua mahitaji watu wa maeneo hayo pamoja na rasilimali zao ili kuwafunza waweze kuzitumia kujenga uchumi na kuboresha maisha yao.

Kwa muktadha huo kuwasaidia kielimu na kiteknolojia kutakuwa na manufaa zaidi kutokana na uanzishwaji wa viwanda vitakavyoajiri watu wanaoishi vijijini na kuzalisha bidhaa kwa ajili ya matumizi yao na kuinua uchumi wao.

Habari Kubwa