Yanga, Azam FC mnaweza kupindua matokeo ugenini

18Mar 2017
Mhariri
Nipashe
Yanga, Azam FC mnaweza kupindua matokeo ugenini

WAWAKILISHI wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa, Yanga na Azam FC wanatarajia kupeperusha bendera ya nchi kati ya leo na kesho wakiwa ugenini kusaka tiketi ya kusonga mbele kwenye mashindano wanayoshiriki.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, yenyewe leo watashuka uwanjani mjini Lusaka, Zambia kuwavaa wenyeji katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika wakiwa na kumbukumbu ya kupata sare ya bao 1-1 kwenye mechi ya kwanza.

Ili iweze kusonga mbele katika mashindano hayo, Yanga iliyoko chini ya Mzambia, George Lwandamina itatakiwa kupata ushindi wowote au sare ya kuanzia mabao 2-2.

Mabingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Azam wao watateremka dimbani kesho kuwakabili wenyeji Mbabane Swallows katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, Azam wao watashuka uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 walilopata hapa nyumbani na sasa wanahitaji ushindi au sare yoyote kwa ajili ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Yanga na Azam wote wanatakiwa kutobweteka na jukumu kubwa walilonalo ni kupambana na kuingia uwanjani kwa ajili ya kusaka ushindi na si vinginevyo.

Ushindi pekee ndani ya dakika 90 ndiyo utawaweka katika nafasi salama ya kusonga mbele kabla ya kufika hatua nyingine ya matuta ambayo mara nyingi makocha husema, ushindi wa penalti ni bahati.

Hakuna kisichowezekana katika soka, lolote linaweza kutokea na wawakilishi hao wanatakiwa kusahau ukweli kauli ya 'Mcheza Kwao Hutuzwa', ushindi katika soka unaweza kupatikana kokote ingawa ugenini wachezaji wanakosa hamasa ya mashabiki wao.

Kilichotokea Ulaya katika mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya kati ya Barcelona na PSG na mchezo kati ya Monaco na Manchester City pia kinaweza kutoka Afrika, kikubwa ni kuingia uwanjani mkiwa na lengo moja la kusaka ushindi na kusahau kilichotokea kwenye mchezo wa kwanza.

Zanzibar mjipange kuandaa timu

BAADA ya Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliofanyika juzi kuridhia Zanzibar kuwa mwanachama kamili, inamaanisha kuwa tayari wamepata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa kuhusisha timu za Taifa (vijana, wakubwa na wanawake).

Tumeshuhudia siku za hivi karibuni, klabu za Zanzibar ambazo zilikuwa zinashiriki katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho zikitolewa hatua ya awali , sasa si wakati wa kuona hayo yanarejea na wanatakiwa kujipanga upya ili kuwa na timu zinazotoa ushindani.

Muda wa kuchanganya siasa na mipira umekwisha, viongozi na wadau wa soka mnatakiwa kuungana na kuimarisha timu zenu ili nguvu iliyotumika ya kuomba uanachama iweze kuonekana ilikuwa na tija.

Habari Kubwa