Yanga ina uwezo wa kuiondoa Zanaco

11Mar 2017
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga ina uwezo wa kuiondoa Zanaco

ZANACO, mabingwa wa soka wa Zambia ni miongoni mwa timu ngumu Afrika kwenye michuano Kimataifa.

Wawakilishi hao kwa sasa wapo hapa nchini kucheza na wawakilishi wa Tanzania Yanga kwenye michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Mchezo huo wa kwanza unachezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya timu hizo hazijarudiana wiki mbili zijazo nchini Zambia.

Pamoja na wawakilishi hao wa Zambia kuwa miongoni mwa timu nzuri Afrika, bado yanga wana nafasi ya kuifunga timu hiyo na kusonga mbele kwa hatua inayofuata ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya vilabu Afrika.

Yanga ni timu nzuri na imekuwa na mafanikio kwa miaka ya karibuni ambapo mwaka jana walifanikiwa kufika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Nipashe tunaamini pamoja na uzuri walionao Zanaco, Yanga ina uwezo wa kupata matokeo mazuri leo kama tu wachezaji wataifanya kazi yao uwanjani kwa asilimia zote.

Yanga ina wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao kama watafuata maelekezo ya kocha wao, George Lwandamina leo wanaweza wakapata ushindi mnono utakaowaweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya mchezo wa marudiano.

Kwa kutambua mashabiki ni sehemu muhimu kwenye mchezo, tunatoa wito kwa mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kuwashangilia Yanga na kuwapa hamasa ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa leo.

Ni wazi ushindi wa Yanga kwenye mchezo wa leo hautakuwa ushindi wao peke yao, lakini pia utakuwa ushindi wa Taifa kwa kuwa timu zinazocheza leo zinaziwakilisha nchi zao.

Lakini pia ni vyema Nipashe ikawakumbusha wachezaji wa Yanga kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja kwenye mchezo wa leo na kuepuka kuondolewa mchezoni na wachezaji wa timu pinzani au mashabiki.

Ni lazima watambue mchezo wa leo utatoa muelekeo wa Yanga kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya Afrika.

Kama watakubali kufungwa kwenye mchezo wa leo watakuwa wamejiweka kwenye wakati mgumu kwa kuwa kutakuwa na mchezo wa marudiano ambao Yanga watacheza ugenini.

Kujiweka kwenye mazingira mazuri ni vyema wachezaji na benchi la ufundi la Yanga wakahakikisha wanapata ushindi mzuri kwenye mchezo wa leo kabla ya kuanza kuupigia mahesabu mchezo ujao wa marudiano.

Nipashe tunaamini Yanga ina uwezo wa kushinda mchezo wa leo kwa kuwa ilifanya maandalizi ya kutosha na pia uwapo wa maelfu ya mashabiki wake kutaongeza hamasa kwa wachezaji.

Ikumbukwe mwaka jana walifika mpaka hatua ya makundi ya michuano ya Afrika, wadau wengi wa soka wanatarajia kuona mafanikio zaidi kwenye michuano ya mwaka huu.

Mathalani hakutakuwa na mafanikio mwaka huu kama Yanga itaondolewa mapema kwenye michuano ya Kimataifa bila hata kufikia hatua ya makundi ambayo waliifikia mwaka jana.

Tutasema Yanga imepiga hatua kwenye michuano hii ya kimataifa kama tu itavuka hatua ya makundi waliyoifikia mwaka jana.

Jambo hilo linawezekana kwa Yanga kama tu watakuwa wameweka malengo hayo na wachezaji kujituma katika kila mchezo.

Nipashe tunawatakia kila heri Yanga kwenye mchezo wa leo tukiamini wanauwezo wa kupata ushindi mbele ya mashabiki wao na kuwapa wakati mgumu Zanaco.

Habari Kubwa