Yanga inaweza wachezaji wakiandaliwa kisaikolojia

02Nov 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga inaweza wachezaji wakiandaliwa kisaikolojia

KESHO wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Klabu ya Yanga watashuka dimbani nchini Misri kucheza mechi yao ya mchujo ya marudiano dhidi ya wenyeji, Pyramids FC kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ambayo iliangukia kucheza mechi hiyo ya mchujo baada ya kutolewa na Zesco ya Zambia kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, katika mchezo huo inahitaji ushindi kuanzia mabao 2-0 ili kuweza kufuzu hatua ya makundi kufuatia mechi ya awali Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kukubali kipigo cha mabao 2-1.

Tayari wawakilishi hao wa Tanzania waliobaki katika michuano ya kimataifa baada ya Simba, Azam, KMC, KMKM na Malindi kutolewa, wapo nchini Misri tangu alfajiri ya jana, hivyo macho na dua zote za Watanzania tunaamini zitakuwa zikielekekezwa kwao ili kuweza kusonga mbele.

Yanga ambayo ilitua nchini Misri alfajiri ya jana, licha ya kupoteza mechi ya kwanza inaweza kupindua matokeo na kusonga mbele pamoja na wengi kuamini kwamba Waarabu hao tayari wamemaliza mchezo baada ya kushinda dakika 90 za awali hapa nchini.

Tunasema inawezekana hasa kutokana na rekodi nzuri ya Yanga ya kutokata tamaa ikiwa ugenini kufuatia kuichapa Township Rollers ya Botswana bao 1-0 ikiwa ni baada ya sare ya 1-1 hapa nchini kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini pia raundi ya kwanza ya michuano hiyo ikatoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa jijini kabla ya kwenda kutolewa kwa tabu na Zesco kwa mabao 2-1, jambo ambalo tunaamini inaweza kufanya makubwa zaidi na kuwashangaza wote wanaoibeza kwa kuona imekwenda kukamilisha ratiba tu kabla ya kurejea kuendelea na Ligi Kuu Bara.

Ingawa wengi wamekatishwa tamaa na kauli ya awali ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera aliyoitoa baada ya Yanga kukubali kipigo cha mabao 2-1 jijini Mwanza dhidi ya Waarabu hao, akieleza kuwa hakuna mchezaji hata mmoja kwenye kikosi chake anayeweza kufananishwa na ubora wa wachezaji wa Pyramids.

Huku pia akienda mbali zaidi kwa kueleza kwamba hakusajili kwa ajili ya michuano hiyo ya kimataifa na kwamba usajili wao ulikuwa maalum kwa michuano ya ndani hususan Ligi Kuu, bado hiyo haiwezi kuwa sababu kwetu kuitoa Yanga mapema kabla ya dakika 90 kukamilika.

Tunatambua Zahera inawezekana alitoa kauli hiyo kutokana na presha kubwa aliyoipata kutoka kwa mashabiki uwanjani hapo waliokuwa wakitamani kuona Yanga ikiibuka na ushindi, lakini pia kitendo cha kurushiwa chupa za maji baada ya matokeo hayo huenda kilichangia na kumpandisha hasira kocha huyo.

Hivyo, ushindi ama kupoteza kwa Yanga kutategemeana zaidi na namna Zahera na uongozi wa klabu hiyo ulivyoweza kuwaandaa wachezaji wa Yanga kisaikolojia kwa kuwaeleza waipuuze kauli hiyo ya kocha kwa kuwa ilitokana na hasira iliyochangiwa na presha kutoka kwa mashabiki.

Nipashe tunatambua itakuwa ni jambo gumu kuwarejesha wachezaji mchezoni, hususan kuwaaminisha kwamba wao ni wa kiwango cha juu na wanaweza kupambana na wapizani wao, lakini tunaamini hao ni kama askari vitani na wanajua ni lazima waamini katika ushindi.

Lakini pia wachezaji hawana budi kuipuza kauli hiyo hasa kwa kutanguliza maslahi yao mbele zaidi na kuonyesha kiwango cha juu kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kutangaza soko lao na kupata klabu kubwa nje ya Tanzania.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba, michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa na utajiri barani Afrika baada ya ile ya Ligi ya Mabingwa, hivyo ni dhahiri kuna mawakala wengi kutoka ndani ya bara hili na nje wanaoifuatilia ili kubaini vipaji, jambo ambalo haitakuwa ajabu kuona miongoni mwa wachezaji watakaoonyesha ubora wakipata soko.

Pamoja na hayo yote, Nipashe tukiwa kama wadau namba moja wa soka hapa nchini, lengo letu ni kuona Yanga ikisonga mbele ili Tanzania iendelee kuwa na nafasi kubwa ya kuvuna pointi na kuweza kuingiza timu nne katika michuano hiyo msimu ujao.

Tunaamini kwa maandalizi Yanga iliyoyafanya, pamoja na kuelewa vema uchezaji wa wapinzani wao kutokana na kukutana katika mechi ya kwanza, itaweza kupindua matokeo kama tu wachezaji watarejeshwa mchezoni kisaikolojia lakini pia nao wakiamini wanapigania maslahi yao binafsi katika mchezo huo, hivyo hatuna budi kuwatakia kila la kheri wawakilishi wetu hao.

Habari Kubwa