Yanga inawezekana, msikate tamaa

25Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga inawezekana, msikate tamaa

INAWEZEKANA wapo waliokata tamaa na mustakabali wa mabingwa wa soka nchini, Yanga SC kwenye mashindano ya kombe la Shirikisho Afrika (CAF) kutokana na kuvuna pointi moja pekee katika michezo mitatu ya kundi A ya michuano hiyo.

Na inawezekana mashabiki na Watanzania wengi wakaona kama Yanga tayari imeshatolewa kwenye mbio za kufuzu kuingia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo kutokana na upishano wa pointi ya timu nyingine kwenye kundi hilo.

Soka ni mchezo wa makosa na mchezo ambao matokeo yake huwezi kuyabashiri kwa asilimia mia moja.

Yanga kesho inacheza mchezo wao wa nne kwenye kundi hilo dhidi ya Medeama nchini Ghana. Kimsingi, ni mchezo mgumu kwa sababu ya ugeni wa Yanga nchini humo.

Nipashe tunaamini kama mpira ni mchezo wa makosa basi hata Yanga bado wana nafasi ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo muhimu kwao.

Ushindi katika mchezo huo utaifanya kufufua matumaini ya kupata nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa ukubwa kwenye ngazi ya vilabu Afrika.

Yanga wanapaswa kufahamu kuwa wapinzani wao watakuwa na wachezaji 11 uwanjani kama wao, hivyo hakuna haja ya kuingia uwanjani na woga wa aina yoyote.

Kila kitu kinawezekana, kikubwa ni namna gani wachezaji wa Yanga watapambana na kuondoa mawazo ya kuwa hawana nafasi ya kusonga mbele kutoka kwenye kundi hilo.

Miaka michache iliyopita, wawakilishi wa Congo Brazzavile, Leopards ikiwa chini ya Kocha wa sasa wa Simba, Joseph
Omog, ilishangaza watu baada ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo wakati kwenye hatua ya makundi ilikuwa katika nafasi kama iliyonayo Yanga kwa kufanya vibaya katika michezo mitatu ya awali.

Wachezaji Yanga wasikate tamaa, bado wanaweza wakashangaza watu kwa kufanya vizuri kwenye michezo iliyobakia na kukata tiketi ya kusonga mbele.

Tunaamni kuwa benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha Hans van Pluijm kwa uwezo na uzoefu alionao kwenye mashindano makubwa, litakuwa limewajenga kisaikolojia wachezaji wao kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Medeama.

Wachezaji wanapaswa kusahau matokeo ya michezo iliyopita, badala yake akili na mawazo yao wavielekeze kwenye mchezo huu ambao tunaamini kama watafanya vizuri, wataamsha morali miongoni mwao na kuendelea kufanya vizuri zaidi kwenye michezo mingine.

Kwa kutambua ni wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano haya, Watanzani wengi wapo nyuma yao wachezaji na timu ya benchi la ufundi.

Nipashe tunawatakia kila heri Yanga kuelekea kwenye mchezo huo muhimu, na tunatambua kuwa bado klabu hiyo ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi kwa kuanzia na Medeama.

Habari Kubwa