Yanga isikate tamaa bado ina nafasi kusonga mbele

13Mar 2017
Mhariri
Nipashe
Yanga isikate tamaa bado ina nafasi kusonga mbele

JUZI ulichezwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wawakilishi wa Tanzania, Yanga dhidi ya Zanaco ya Zambia.

Mchezo huo uliisha kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 huku Yanga wakiwa wa kwanza kupata goli kupitia kwa mshambuliaji wake nyota, Simon Msuva.

Kwa ujumla, matokeo hayo yanaonekana kuibeba zaidi Zanaco na kuwa si mazuri kwa Yanga.

Hata hivyo, Nipashe linafahamu kuwa Yanga bado ina nafasi ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki ijayo nchini Zambia.

Hakuna sababu ya Yanga kukata tamaa kwa matokeo hayo ya sare.

Kama kutakuwa na malengo na juhudi za dhati kutoka kwa wachezaji na benchi la ufundi, Yanga ina uwezo wa kuyabadilisha matokeo waliyoyapata juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Jambo la msingi ni kwa Yanga kujitambua na kufanya tathmini ya mchezo uliopita kufahamu wapi ilikosea na kupata matokeo hayo ya sare.

Hakika Nipashe tunafahamu yapo makosa ya kiufundi ambayo yameifanya Yanga kushindwa kupata ushindi kwenye mchezo huo wa juzi.

Kwa mfano, Zanaco ilikuja nchini ikitambua wazi kuwa Yanga ina mshambuliaji wanayemtegemea Donald Ngoma.

Walinzi wa Zanaco walikuwa wakicheza kwa tahadhari kubwa huku wakihakikisha hawampi nafasi Ngoma.

Mabadiliko ambayo Yanga iliyafanya kwa kumtoa Ngoma, yaliwapa ahueni mabeki wa Zanaco na kuanza kusaidia mashambulizi ya timu yao na kusababisha kupata bao hilo muhimu ambalo linaweza kuwabeba kwenye matokeo ya jumla baada ya mchezo wa marudiano.

Hata hivyo, Yanga hawapaswi kukata tamaa, bado wana nafasi ya kuwatoa Zanaco na kusonga mbele kwenye michuano hii.

Benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha George Lwandamina, wanapaswa kufanya tathmini ya mchezo uliopita na kuandaa mbinu zitakazowawezesha kupata ushindi kwenye mchezo wa marudiano.

Kama Zanaco wamepata bao moja hapa ugenini, basi ni wazi hata Yanga wanaweza wakapata bao au mabao kwenye mchezo wa marudiano.

Cha msingi wachezaji wa Yanga wanapaswa kufahamu kuwa wanatakiwa kupambana kwenye mchezo wa marudiano pasipo kuwaogopa wapinzani wao.

Inawezekana Yanga ilikuwa haiifahamu vizuri Zanaco, lakini kwa mchezo wa juzi ni wazi sasa wanawafahamu na wataandaa mikakati ya kuwafunga kwa kuwa wameona mbinu zao.

Nipashe tunaisisitiza Yanga, isikate tamaa kwani kazi haijaisha.

Mchezo wa marudiano Zanaco watakuwa na wachezaji 11 uwanjani, hivyo hivyo Yanga pia watakuwa na wachezaji idadi kama hiyo.
Kwa mantiki hiyo, Yanga inapaswa kujiamini na kujipa moyo kuwa ina uwezo wa kusonga mbele.

Jambo la msingi kwa Yanga sasa ni kuanza maandalizi ya mchezo wa marudiano mapema.

Tunaitakia Yanga kila kheri kwenye mchezo wa marudiano na kikubwa wafahamu kuwa bado wana nafasi ya kusonga mbele kama tu watapambana na kujitolea kwa dhati uwanjani.

Habari Kubwa