Yanga, JKU ushindi mnono lazima leo

13Feb 2016
Mhariri
Nipashe
Yanga, JKU ushindi mnono lazima leo

LEO, timu za Yanga na JKU ya Zanzibar zinaanza kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa Klabu Bingwa Afrika.
JKU watakuwa nyumbani, Uwanja wa Amaan, Zanzibar kucheza dhidi ya AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mabingwa wa Bara, Yanga wanaanza ugenini nchini Mauritius kupambana na wenyeji wao Cercle de Joachim.

Michezo hiyo yote inabeba matumaini ya mashabiki wa soka nchini, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishuhudia timu zao zikiaga mashindano mapema.

Nipashe tunaamini uwezo wa timu hizi mbili, Yanga na JKU kufanya vizuri upo kama watapambana kama watapambana mwanzo mwisho.

Ni lazima kupambana kwa nguvu zote kwa sababu mashindano haya yana hadhi kubwa kwa ngazi ya klabu Afrika, hivyo timu zinazofuzu zina uwezo wa kutosha.

Tunachukua nafasi hii kuwakumbusha wachezaji wa timu zote mbili kupeperusha vizuri bendera ya nchi kwenye mashindano hayo.

Tusingependa kuona timu zetu zinapeperusha bendera katika namna ya kushiriki na siyo kushindana.

Katika mashindano makubwa kama haya, timu inayofanya vizuri ndiyo ambayo hujitangaza kimataifa pamoja na wachezaji wake.

Wawakilishi wetu watakapoingia uwanjani, wajue wana deni kubwa la kuwalipa Watanzania waliochoka kila mwaka kuwa wasindikizaji.

Ni jukumu la wachezaji wetu kuhakikisha wanafanya kile walichoelekezwa na walimu wao ili kupata matokeo mazuri.

Kwa upande wa Yanga inayoanza ugenini, tunawakumbusha wachezaji kuacha kucheza kwa kujiami zaidi badala ya kushambulia na kutafuta ushindi mnono.

Mfumo wa kucheza kwa kujiamini zaidi ugenini na kutegemea kushambulia wakati wa mechi ya marudiano, kunaweza kusiwe na msaada.

Wachezaji wa Yanga wahakikishe wanazitumia vizuri kufunga nafasi zote watakazopata ili kurudi nyumbani na ushindi mnene utakaowahakikishia urahisi wa kusonga mbele.

Nipashe, tunaamini kuwa maelekezo ya mwalimu yatakuwa kiini cha ushindi wa mabao mengi kwenye mchezo huo, lakini tu kama wachezaji watakuwa tayari kuyafuata.

Tunategemea Yanga watarejea nchini na ushindi mkubwa na kujihakikishia nafasi ya kusogea hatua ya pili ya michuano hiyo.

Kwa wawakilishi wa Zanzibar, ambao pia ni sehemu ya Tanzania, nao wanapaswa kuutumia vizuri uwanja nyumbani kupata ushindi mkubwa.

Hakuna nafasi nyingine muhimu ya kucheza mbele ya mashabiki zaidi ya Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Hivyo basi, wana kila sababu ya kutumia vizuri kufunga bao katika kila nafasi watakayopata.

Tuchukue nafasi hii pia kuwakumbusha wawakilishi wetu kwamba, kwenye mchezo wa soka hakuna timu ndogo au nchi ndogo.

Kuna uzoefu umewahi kutengeneza rekodi na kuandika historia kwa timu ndogo kufanya vizuri kwenye mashindano makubwa ya aina hii.

Hivyo basi, ni vizuri wachezaji wetu wakazingatia hayo na kujituma uwanjani, huku pia wakiweka nidhamu mbele. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Yanga na JKU.