Yanga maandalizi kuivaa Pyramids yaanze mapema

12Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga maandalizi kuivaa Pyramids yaanze mapema

BAADA ya droo ya mechi ya hatua ya mtoano ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika tangu Jumatano iliyopita, na Yanga kupangwa na Pyramids ya Misri, inamaanisha kuwa maandalizi kuelekea mchezo huo yanatakiwa yaanze sasa.

Yanga ambao ndio wawakilishi pekee wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wataanza kwa kuwakaribisha Waarabu hao hapa nyumbani Oktoba 27 mwaka huu, na mchezo wa marudiano utachezwa Novemba 2 mwaka huu huko nchini Misri.

Ili kuhakikisha kuwa Yanga inafanya vema na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo, inahitaji kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo ya kwanza huku ikijiandaa kwenda kukamilisha ratiba huko ugenini.

Waswahili wanasema siku hazigandi, huu ndio muda muafaka wa Yanga kuanza maandalizi ya mechi hizo mbili za kimataifa, ambazo kama Yanga watafanikiwa kushinda, watakuwa wametinga hatua ya makundi ambayo itawaletea sifa kama klabu, vile vile itawapatia fedha.

Mbali na kuipa sifa klabu, tayari Yanga watakuwa wameipeperusha vema bendera ya Tanzania katika mashindano hayo yanayofanyika kila mwaka kama walivyofanya watani zao, Simba kwenye msimu uliopita, ambao walifika hatua ya robo fainali.

Tunapenda kuwakumbusha viongozi, benchi la ufundi, wachezaji na wadau wote wa Yanga, huu ndio wakati wa kushikamana na kushirikiana kuhakikisha timu yenu inasonga mbele katika michuano hiyo na kuendelea kuipa Tanzania Bara pointi ambazo zitafanya iendelee kuwakilishwa na klabu nne katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.

Tunaamini kuwa timu iliyofanya maandalizi mazuri, ina nafasi kubwa ya kupata matokeo chanya na huu ndio wakati sahihi wa Yanga kujipanga kuwasoma wapinzani wenu ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuwafunga.

Nipashe linawakumbusha Yanga kuwa, kwenye dunia ya sasa, hakuna timu ndogo au kubwa, timu zote zilizofika hatua ya mtoano, zina hadhi na viwango vinavyofanana. Ila mshindi wa jumla katika mechi hizo mbili mtakazocheza, ndio atakuwa bora.

Ni vema wahusika wote muhimu, mkaanza mapema maandalizi ya kuhakikisha mnafanya vema katika dakika hizo 180 zinazowasubiri, lakini mkifanya vizuri zaidi katika dakika 90 za kwanza hapa nyumbani.

Ushindi wa nyumbani, utawafanya wachezaji kuwa na morali na ari ya juu ya kwenda kumalizia kazi waliyoianza huko ugenini na si kujiweka katika "mlima mrefu" au kusema wanakwenda "kupindua meza" kama ilivyozoeleka.

Huku ikitumia mechi zake za ligi dhidi ya Alliance na Mbao FC itakazocheza (kama ratiba ya Ligi Kuu Bara iliyopo) kabla ya kuikaribisha Pyramids, haitabadilika kujiandaa kuwavaa Waarabu hao, ni vema pia ikawa na programu nyingine maalumu ya kuhakikisha wachezaji wake wanaandaliwa kushinda mchezo huo wa kimataifa.

Kuelekea mchezo wa kwanza dhidi ya Pyramids, Yanga inatakiwa iingie uwanjani ikiwaheshimu wapinzani wao na vile vile ikiufananisha mchezo sawa na fainali, hivyo inatakiwa kupata ushindi mnono ambao utawaweka kwenye nafasi salama na nzuri ya kusonga mbele.

Kama Simba iliweza kuwavua ubingwa vigogo Zamalek, Yanga pia inaweza kuwaondoa Pyramids ambayo ina miaka 11 tangu ilipoanzishwa na kamwe isitishwe na majina au nchi wanazotoka wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ambacho kiko katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Misri.

Hakuna kisichowezekana, endapo Yanga itafanya maandalizi mazuri na mapema, itasonga mbele katika michuano hiyo na kuwapa furaha mashabiki wake ambao waliumia baada ya kuona wametolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Zesco ya Zambia.

Habari Kubwa