YANGA MSIBWETEKE, KAZI BADO

28May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
YANGA MSIBWETEKE, KAZI BADO

MSIMU huu ni timu pekee iliyofanya vizuri zaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, imefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara, imetwaa kombe la Shirikisho (FA) na kikubwa zaidi imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michunao ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

Hiyo inaonyesha Yanga imepata mafanikio zaidi miongoni mwa timu za Afrika Mashariki, Nipashe tunaamini mafanikio hayo yamepatikana kutokana na kujituma kwa wachezaji kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi na pia uongozi imara umesaidia kwa kiasi kikubwa Yanga kufika hapa ilipo sasa.

Nipashe inatoa angalizo au ushauri kwa wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo, kazi ndio imeanza, wanatakiwa
kuacha kasumba za timu zetu za hapa Tanzania kubweteka pale wanapoona wamepata mafanikio kidogo.

Michuano ya Shirikisho Afrika ni mashindano makubwa na timu zote ambazo zimefanikiwa kutinga hatua hiyo ya makundi ni timu kubwa Afrika hivyo Yanga ni lazima ijitathimini na kufanya maandalizi ya mapema na kuacha kufikilia kama kazi wamemaliza.

Kama ni safari basi Yanga ndio mmeianza sasa hivi, kikubwa uongozi na benchi la ufundi liendelee na mipango ya kuhakikisha timu inafanya vizuri kwenye hatua hiyo.

Ni kipindi cha mwezi mmoja tu kimebakia kabla ya kuanza hatua hiyo ya makundi ambapo Yanga itaanzia ugenini nchini Algeria, Nipashe tunashauri maandalizi ya mchezo huo yaanze sasa hivi na wachezaji wasipewa mapumziko ya muda mrefu kama wanataka kufanya vizuri.

Wachezaji wengi wa Tanzania hawawezi kutunza mazoezi yao, hivyo kuwapa mapumziko ya muda mrefu kunaweza kuchangia kushusha viwango vyao katika kipindi hiki muhimu kuelekea michezo ya hatua ya makundi.

Ni vyema kocha mkuu akaendelea na mikakati yake mara moja hasa baada ya kufanikiwa kutwaa kombe la Shirikisho wiki hii.

Nipashe tunaamini maandalizi mazuri yataisaidia Yanga kufanya vizuri zaidi, na lazima wachezji, viongozi na benchi la ufundi lifahamu kuwa wapinzani wao wameanza kuwafuatili kutaka kujua mambo mbalimbali hasa mbinu zao.

Na kwa mantiki hiyo hiyo, huu ni wakati mzuri kwa benchi la ufundi la Yanga kuanza kufuatilia mikanda ya video ya timu pinzani walizopangwa nazo kwenye michuano hiyo.

Hii itasaidia Yanga kuwafahamu vyema wapinzani wao hasa kwa kuzingatia hawajakutana na timu hizo kwa miaka ya karibuni au pengine hawajakutana kabisa zaidi ya kuzisikia.

Soka la sasa ni la mbinu na mipango mingi, Yanga msibweteke ni wakati wa kusaka mbinu na mipango ya kuzimaliza timu pinzani mtakazokutana nazo.

Mafanikio ya kutwa makombe mawili msimu huu na kufika hatua ya makundi iwe chachu ya kufika mbali zaidi kwa kuhakikisha mnaibuka vinara kwenye kundi lenu.

Nipashe tunatakia kila la heri katika maandalizi ya michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya vilabu barani Afrika.

Habari Kubwa