Yanga Princess, Simba Queens mechi 'darasa'

08Jan 2022
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga Princess, Simba Queens mechi 'darasa'

LIGI Kuu ya Wanawake Tanzania imeingia katika raundi ya nne na leo mashabiki wa soka wanatarajia kushuhudia mechi itakayowakutanisha watani wa jadi hapa nchini, Yanga Princess dhidi ya wageni, Simba Queens, wote kutoka jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa msimu huu wa 2021/22 na inatarajiwa kuchezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru jijini.

Kama ilivyo kaka zao Simba na Yanga wanapokutana, 'joto' kutoka kwa viongozi, wachezaji na mashabiki hupanda, vile vile hali hiyo imeanza kuonekana wakati 'kinadada' hao wanapokutana katika mechi hizo za ligi.

Simba Queens iliyotangulia kupanda daraja, imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya watani zao, ikitoa vichapo katika michezo yote miwili katika msimu wa 2019/2020 halafu ikatoka sare na kushinda mchezo wa marudiano msimu uliopita na leo watakutana kwa mara ya tano tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo.

Mabingwa watetezi, Simba Queens watashuka dimbani wakiwa kileleni baada ya kushinda mechi zake tatu zilizotangulia, tena kwa idadi nono ya mabao wakati Yanga iko katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 12 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Mbali na kila timu kuhitaji ushindi ili kuendelea kujiimarisha katika vita ya kuwania ubingwa, lakini mechi hii inachukuliwa kama 'kioo' cha soka la wanawake hapa nchini.

Timu zote mbili zimeboresha vikosi vyao, ingawa kila timu imeondokewa na nyota wake waliokuwa katika kikosi cha kwanza msimu uliopita, Simba Queens ikiuza nje ya nchi wakati Yanga Princess ikizidiwa dau na klabu nyingine za hapa hapa Tanzania zilizojipanga kuonyesha ushindani.

Mechi ya leo ina mambo mbalimbali ya kujifunza kuanzia kwa wachezaji, makocha pamoja na wadau wote wa soka nchini ambao wamekuwa wakihudhuria michezo mingine ya wanaume.

Kwa sababu mechi hii inatarajiwa kuonyeshwa mubashara na Kituo cha Azam Media, basi wachezaji wahakikishe wanacheza kwa viwango vya juu ili kutumia fursa ya mchezo huo kutangaza vipaji walivyonavyo kama ambavyo wanaume wanavyofanya.

Tunawakumbusha wachezaji wa Simba Queens na Yanga Princess kuibeba heshima ambayo wanaipata ya kuonekana mubashara, ripoti zinasema hakuna nchi nyingine Afrika ambayo mechi za Ligi ya Wanawake zinaonyeshwa mubashara, kwa maana hiyo nafasi ambao wamezipata timu hizi itendewe haki.

Kila mchezaji anatakiwa kufahamu mbali na kuonekana wakiwa na timu za Taifa (Twiga Stars na Tanzanite), mchezo huu ni daraja lingine kwao la kuwashawishi mawakala na makocha kuwatafutia timu katika mataifa mengine ya Afrika au barani Ulaya.

Kama imewezekana kwa Mwanahamisi Omary 'Gaucho' na Enekia Lunyamila kusajiliwa huko Morocco, basi ule mchakato wa mshambuliaji wa Simba Queens, Oppa Clement kuelekea Israel na wengine kuonekana unaweza kutimia endapo watajituma na kuonyesha kandanda safi.

Tunaamini ili ndoto za wachezaji hawa kwenda kucheza soka la kulipwa zitimie, ni lazima waonyeshe nidhamu na si kila mchezaji ataibeba timu yake, lakini atawaachia 'maswali' wafuatiliaji wa mechi hiyo na hatimaye kile kilichowachelewesha kwenda kusakata kandanda ya kulipwa kikamalizika.

Nidhamu itakayoonyeshwa si tu itawajenga wachezaji, lakini pia itasaidia kuwavutia wadhamini ambao wanahitajika katika kusaidia maendeleo ya soka la wanawake hapa nchini.

Ni imani yetu makocha waliopewa dhamana ya kuziongoza timu hizo mbili, Edna Lema kwa upande wa Yanga Princess na Sebastian Mkoma anayewaongoza mabingwa watetezi, kuwatendea haki mashabiki wao kwa kupanga vikosi vitakavyoonyesha soka safi kutokana na vipaji walivyonavyo wachezaji wa timu hizo mbili.

Pia tunaamini waamuzi watakaopewa dhamana ya kuichezesha mechi hiyo watatafsiri vyema sheria zote 17 za mchezo huo ili timu itakayostahili kupata ushindi au sare ipate.

Habari Kubwa