Ziongezwe juhudi zaidi kuwahudumia wazee

22Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ziongezwe juhudi zaidi kuwahudumia wazee

TAARIFA kuwa baadhi ya halmashauri na manispaa nchini zinatenga fedha kwa ajili ya kutengeneza vitambulisho vya matibabu ya wazee yanayoelezwa kuwa yatatolewa bure, zinatia moyo.

Wazee ambao wamelitumikia taifa hili kwa miaka mingi wamekuwa waathirika wa kukosa huduma za matibabu.

Licha ya kuwa na juhudi na vitambulisho hivyo, wazee wanakabiliwa na usumbufu unaowasababishia kukosa huduma kwa vile wengi hawana fedha na hawana msaada.

Ni sawa, halmashauri kutenga fedha na kuwaandalia vitambulisho lakini, suala la usumbufu ukiwamo kupewa barua za watendaji wa serikali za mitaa na barua za Idara za Ustawi wa Jamii za hospitalini wanapotakiwa kufanyiwa vipimo na kupata huduma za kibobezi zinawakatisha tamaa zaidi.

Itoshe kusema kuwa mzee atambulike kwa kitambulisho cha taifa alicho nacho ambacho kinaainisha taarifa zake zote, kuanzia umri, kabila, makazi na shughuli zake.

Mara nyingi wazee wanapokwenda hospitalini kusaka tiba wanalazimika kupitia kwa ofisa za serikali za mitaa.

Ni sawa na utaratibu bora wenye malengo mema, lakini mara nyingi ni usumbufu. Si hivyo tu ni kama kuwapa usumbufu wa ziada kwa vile wanafahamika kutokana na kadi za utambulisho walizo nazo.

Pengine suala la kuomba tena kupata msamaha wa matibabu kwenye ofisi za Ustawi wa Jamii hospitalini ni usumbufu mwingine usio na sababu wanaopitia wakati wakifuatilia vipimo vikubwa kama CT - Scan na MRI au Ultrasound.

Wakati mwingine tunashawishika kusema kuwa hakuna sababu ya kuwa na vitambulisho hivyo. Pengine wangetumia vitambulisho walivyo navyo kama vile vya kupigia kura au vya utaifa.

Taarifa hizo zinaweza kutosha kumtambulisha mtu kuwa ni mzee, yote hayo yakifanyika ili kuwaepushia usumbufu usio na sababu hasa kwenye kuwafikia madaktari bingwa na wabobezi.

Licha ya serikali kufanya jitahidi mbalimbali kutatua changamoto lukuki zinazowakabili wazee hasa kwa upande wa matibabu, upatikanaji wa dawa ni matatizo yananayowakabili watu wazima hawa.

Mara nyingi wazee wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa matibabu hasa dawa kwa vile wapo wasio na uwezo wa kununua.

Wazee wengine wanaona kuwa licha ya kupewa vitambulisho hivyo vya matibabu bure, lakini wanapokwenda hospitalini mara nyingi huambiwa hakuna dawa.

Tunaona kuwa ni wakati wa kuwa na dirisha la wazee lakini, pia kuanzisha kanzi data yenye taarifa zao, kama ilivyo kwa daftari la wapiga kura.

Licha ya kwamba baadhi ya hospitali zimeshatenga madirisha ya wazee kwenye huduma za afya ni wakati wa kuwa na madirisha hayo katika hospitali za mikoa na rufani.

Aidha, tunashauri kuwa ni vyema pia kuwa na maduka ya dawa za wazee ikichukuliwa kuwa magonjwa ya uzeeni yanahitaji tiba muhimu na yana gharama kubwa na hata kutumia wabobezi.

Wazee husumbuliwa na matatizo ya moyo kupanuka, maradhi ya mifupa, mishipa ya fahamu na wakati mwingine saratani.

Magonjwa hayo yanachunguzwa kwa vipimo vya gharama kubwa na wakati mwingine wagonjwa wanakutana na misururu mirefu ya kungojea matibabu (appointment).

Kwa hiyo ni wakati wa kuwafikiria wazee na kuona uwezekano wa wakuwaondoa kwenye misururu hiyo.

Kuwapa vipaumbele kwenye vipimo vya MRI, CT-Scan na tiba nyingine zenye misururu ya kuwafikia wabobezi ni jambo muhimu kwenye kuwahudumia wazee na kuwapa tiba kwa utaratibu rafiki.

Baadhi ya huduma ambazo pengine watu wanalazimika kuzichangia itabidi serikali kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii, izipatie ufumbuzi wa namna ya kuzipata ili kuwasaidia wagonjwa hao.