Mawaziri bila kutoa majibu, ziara zenu ni bure

13Jan 2016
Nipashe
Mawaziri bila kutoa majibu, ziara zenu ni bure

RAIS John Magufuli baada ya kuingia Ikulu, alipiga marufuku watendaji wa serikali kufanya safari za nje ya nchi zisizokuwa na tija kwa taifa.

Naamini alifanya hivyo kwa nia njema na iliyo lenga kubana matumizi ya serikali.
Kwa bahati nzuri sijasikia hawa watendaji wakitoka nje ya nchi kikazi na hii inaonyesha kwamba wametii agizo la Rais Magufuli.
Badala ya watendaji wa serikali wakiwamo Mawazi na Manaibu wao kutii agizo la bosi wao wameamua kuelekeza nguvu katika kufanya ziara za ndani katika mikoa mbalimbali.
Wengi wametoka Dar es Salaam na kwenda mikoani kuwaona wananchi na kusikiliza matatizo yao kwa nia njema kabisa ya kuyapatia ufumbuzi wa kudumu ama wa muda.
Lakini katika ziara zao, hawa Mawaziri inaonekana kama vile wanakwenda kujifunza kila kitu na kuishia kutoa ahadi ama kutishia kuwafukuza ama kuwasimamisha kazi walio chini yao huko mikoani.
Kitendo cha hawa Mawaziri kufika kwa wananchi na kushindwa kuwasaidia wananchi na kuonekana kama vile wameenda kujifunza kila kitu hakiwezi kuwasaidia wananchi.
Kwa mfano Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa alikwenda mkoani Ruvuma akakuta wagonjwa wakiwa wamelala wawili katika kitanda kimoja kwenye wodi ya hospitali moja halafu akaonekana kushangaa.
Wagonjwa kulala chini ama wawili kutokana na uhaba wa vitanda katika hospitali siyo jambo la kumshangaza Waziri Mkuu na kuonekana kama vile alienda huko kujifunza.
Haiwezekani akawa hajui tattizo la uhaba wa vitanda katika nchi hii, hili ni jambo la kawaida na wala mtu hahitaji kwenda shule wala kufanya utafiti ili kulibaini.
Kabla hili la Waziri Mkuu halijapoa, Waziri mwingine akaenda wilaya ya Masasi hivi karibuni kwa ajili ya kutembelea hospitali naye akakuta hali ni hiyo hiyo ya wagonjwa kulala chini ama kulala wawili katika kitanda kimoja.
Kwa bahati mbaya na yeye akaonekana kama vile alienda huko kujifunza, lakini swali la kujiuliza hapa hivi ni kweli hawa viongozi hawajui chochote kuhusu matatizo yanayozikumba hospitali mbalimbali hapa nchini yakiwamo ya uhaba wa dawa, vitanda, miundombinu mibovu ama watendaji?
Haikuishia hapo, juzi Waziri Jenista Mhagama naye alikwenda mkoani Simiyu kuangalia wananchi waliokubwa na baa la njaa, lakini na yeye akaonekana kana kwamba alienda kujifunza.
Akasema ameona ukubwa wa tatizo na anarudi kujipanga ikiwamo kuwambia watendaji wake waharakishe kupeleka chakula cha msaada huko Simiyu.
Waziri Mwigulu Nchemba naye alikwenda eneo la Dumila mkoani Morogoro akakuta mauji ya mifugo yaliyofanywa na wakulima wa eneo hilo.
Nchemba alifika akashuhudia mizoga ya ng'ombe ikiwa imelala chini, lakini akageuka na kurudi Dar es Salaam kwa kuwa hakuwa na mjibu na kwa lugha nyepesi na yeye kama vile alikuwa amekwenda kujifunza kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji.
Hii tabia ya hawa Mawaziri wachache na wengine kwenda mikoani kijifunza kila kitu nadhani siyo sahihi, wafike mahali sasa waende kutatua kero na kuzimaliza.
Kama hawana uwezo wa kutatua kero za wananchi kwa wakati huo, wajitahidi kufanya mawasiliano na watendaji wenzao huko mikoani ama wizarani na kujipa muda kidogo ili kutafuta majibu kabla ya kwenda huko.
Inawaumizi sana wananchi pale wanapomuona kiongozi kama Waziri anafika kwao na yeye anabaki anashangaa na kuanza kujifunza badala ya kutoa majibu.

Ili Waziri awe kiongozi mzuri anapaswa kuwa mtu anayebeba majibu kwenye mkoba wake, lakini siyo mtu anayekwenda kuungana na wananchi kuendelea kulalamika.
MWISHO

Licha ya kuonekana hawa Mawaziri wanafanya mambo mengi kwa mtindo wa kujifunza, lakini hata maagizo wanayotoa sina hakika kama wanarudi kuangalia utekelezaji wake.

Kama hilo halitafanyika hizi ziara mikoani ambazo zinashuhudiwa Mawaziri wakipishana hazitakuwa na maana yoyote kwa wananchi.
Mawaziri hawa najua wanafanya kazi kwa bidii wakiwa wameambatana na waandishi wa habari kwa lengo la bosi wao ambaye ni Rais awaone, lakini atawaona vizuri zaidi kama watakuwa wanakwenda kwa wananchi wakiwa na majibu ya kero zinazowakabili.

Habari Kubwa