Mawaziri watoswa msafara wa Magufuli

24Jan 2016
Nipashe Jumapili
Mawaziri watoswa msafara wa Magufuli

MAWAZIRI wa serikali ya awamu ya tano wameendelea kubanwa kutosafiri nchi za nje ambapo safari hii wametoswa kwenye ujumbe wa Rais John Magufuli nchini Botswana, alikowakilishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

rAIS john magufuli na Waziri Mkuu, Kassim MAJALIWA

Katika msafara huo, Waziri Mkuu hakuambatana na Waziri wala Naibu Waziri yoyote na badala yake alikwenda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi, Job Masima pekee.
Ulikuwa mkutano wa viongozi wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambao ulijadili hali ya usalama ya Lesotho.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili imezipata kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu zinasema kwenye msafara huo hakukuwa na Waziri hata mmoja kama ilivyozoeleka kwenye misafara ya aina hiyo wakati wa utawala wa awamu ya nne wa Jakaya Kikwete.
“Hakukuwa na Waziri yoyote kwenye msafara wa Waziri Mkuu," alisema mmoja wa maofisa waliokuwa kwenye msafara huo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
"Ni Katibu Mkuu mmoja tu na msafara (mzima)... hakukuwa na watu wengi kama zamani… hilo ndilo naloweza kukwambia.”
Hatua ya Waziri Mkuu, kusafiri kwenye mkutano mkubwa bila kuwa na Waziri hata mmoja ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la kupunguza matumizi ya serikali kwa kuhakikisha watumishi wa umma wanaosafiri ni wale tu ambao wanalazimika.
Marais waliohudhuria mkutano huo ni mwenyeji Ian Khama, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi wakati Zimbabwe iliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Simbarashe Mumbengengwi.
Ilikuwa kawaida kwenye serikali ya awamu ya nne msafara wa rais kama huo wa Gaborone Botswana kwenda na ujumbe wa watu hadi 20 hali ambayo Rais wa awamu ya tano, Magufuli aliwahi kuielezea kuwa ilikuwa ikichangia kufuja mabiloni ya fedha za umma.
Tangu aingie Ikulu siku 80 zilizopita, Rais Magufuli hajawahi kwenda nje ya nchi baada ya kuwakilishwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwenye kongamano la kibiashara la China na wakuu wa nchi za Afrika nchini Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka jana.
Agizo la kuwazuia watumishi wa serikali kusafiri nje lilitolewa na Rais Magufuli siku moja baada ya kuapishwa, lengo ikiwa ni kubana matumizi ya serikali na hadi sasa ameshaokoa zaidi ya Sh. trilioni 1.5.
Akilihutubia Bunge la 11 na kulizindua mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli aliwataka watanzania na wabunge waunge mkono uamuzi wake wa kupiga marufuku safari za nje ili fedha hizo zitumike kwenye huduma za jamii kama barabara, afya na elimu.
Alitoa mfano kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2013 na nusu ya 2014/2015 pekee, safari za nje ya nchi ziligharimu Sh. bilioni 356.3 fedha ambazo alisema zingeweza kujenga barabara yenye urefu wa Kilomita 400 au miradi mbalimbali ya jamii.
Alisema tiketi za ndege pekee ziligharimu Sh. bilioni 183.160, mafunzo ya nje ya nchi Sh. bilioni 68.612 na posho za kujikimu Sh. bilioni 104.552.
Mwishoni mwa mwaka jana, Rais Magufuli aliwahi kuagiza maofisa wanne wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza kumwakilisha katika mkutano wa Jumuiya ya Madola uliofanyika visiwa vya Malta, badala ya ujumbe wa watu 50 kama ilivyokuwa imezoeleka.
Mbali na safari za nje, Rais Magufuli amedhibiti pia safari za ndani kwa kuagiza vikao vya kikazi baina ya viongozi wa mikoa vifanywe kwa teknolojia ya video (Video Conference) na wasisafiri kutoka mkoa mmoja na kwenda mwingine wala kukodi ukumbi wa mikutano.
Desemba 17 mwaka jana, Rais aliagiza kusimamishwa kazi watumishi wanne wandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) - Doreebn Kapwani, Mary Mosha, Ekwabi Mujungu na Rukia Nikitas ambao walisafiri bila kuwa na kibali cha Ikulu.

MAAZIMIO YA MKUTANO WA GABORONE
Miongoni mwa maazimio ya mkutano huo ni serikali ya Lesotho kufanyia marekebisho mifumo yake ya usalama na kuandaa ramani ya utekelezaji wa mageuzi ya mifumo yake ya usalama kama ilivyopendekezwa kwenye ripoti ya mwisho ya viongozi wa SADC.
Maazimio mengine ya mkutano huo ambao Rais Magufuli aliwakilishwa na Majaliwa ni kuitaka Lesotho kutoa taarifa ya maendeleo ya maazimio hayo kwenye mkutano wa viongozi hao utakaofanyika Agosti mwaka huu.
Mkutano huo pia uliazimia kwamba serikali ya Lesotho na wadau wengine wa nchi hiyo waweke mazingira mazuri yatakayosaidia wanachama wa vyama vya upinzani na wanajeshi wa nchi hiyo walioko uhamishoni kurudi nchini mwao bila kunyanyaswa.

Habari Kubwa