Maxime: Zamu yetu kutwaa Mapinduzi Cup

13Jan 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Maxime: Zamu yetu kutwaa Mapinduzi Cup

MTIBWA Sugar leo inacheza fainali ya Kombe la Mapinduzi mara ya tano tangu mwaka 2007, pale itakapoivaa URA ya Uganda kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.

Kikosi cha Mtibwa

Mtibwa wamecheza fainali ya Kombe la Mapinduzi mara nne sawa na mabingwa wa kihistoria Simba, lakini vijana hao wa Morogoro wametwaa taji mara moja mwaka 2010.
Mechi hiyo kali itakayochezwa kuanzia saa 2 usiku inazikutanisha timu zilizofuzu hatua hiyo baada ya kuzifunga timu zilizokuwa zikipewa nafasi kubwa, wakiwamo mabingwa watetezi, Simba waliofungwa bao 1-0 na Mtibwa na Yanga waliofungwa kwa mikwaju ya penalti na URA.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alisema anatambua ugumu wa mechi hiyo na kwamba vijana wamejipnga kuandika rekodi mpya.
Alisema: "URA ni timu nzuri hasa nafasi ya kiungo, tumejiandaa kuwakabili kwa namna atakavyokuwa wakicheza.
"Wapinzani wetu wanacheza Ligi Kuu Uganda ambayo kiushindani ni ngumu kuliko ligi yetu, hivyo lazima wawe wazuri.
"Mechi itakuwa ngumu, wanachezesha vikungo wengi katikati na hawaonekani kuwa na haraka. Katika staili kama hii, lazima kucheza kwa makini zaidi."
Alisema wachezaji kama Kyeyuna Saidi, Nkugwa Elkannah na Oscar Agaba ni miongoni mwa wanaotakiwa kuchungwa sana.
Alisema wamejiandaa kulinda heshima ya Watanzania baada ya timu nyingine za hapa nyumbani, Simba, Yanga na Azam kutolewa.
Kocha wa URA, Kefa Kisala aliliambia gazeti hili jana kuwa wanaipa umuhimu mkubwa michuano hiyo na kwamba wako Zanzibar siyo kushiriki, bali kushindana na kutwaa taji.
Kisala alisema kuwa wanaifahamu Mtibwa Sugar na wamejiandaa kucheza kwa umakini kutokana na ugumu wao.
Nahodha wa URA, Simeon Massa alisema watapambana kwa nguvu zote kuhakikisha wanarudi nyumbani na taji.
Bingwa wa mashindano hayo atapata zawadi ya Sh. milioni 10 na mshindi wa pili atajinyakulia Sh. milioni 5.

Habari Kubwa