Mazembe, Genk zavutana uhamisho wa Samatta

19Jan 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
Mazembe, Genk zavutana uhamisho wa Samatta

Jamal Kasongo, wakala wa Mwanasoka Bora wa Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza barani, Mbwana Samatta, amesema kuwa bado kuna mvutano wa kimaslahi kati ya TP Mazembe na klabu Genk licha ya straika huyo kusaini kuichezea klabu hiyo ya Ubelgiji.

MBWANA SAMATTA

Kasongo alikaririwa na moja ya vituo vya redio vya jijini Dar es Salaam jana akieleza kuwa licha ya Samatta kuafikiana na Genk, mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi, bado anavutana na klabu hiyo hasa kwenye suala la fedha za uhamisho.
"Inavyoonekana TP Mazembe hawajaafiki kiasi cha fedha ambacho Genk wanataka kulipa kwa ajili ya Samatta, bado pande mbili hizo zina mvutano ila ninaendelea kulifuatilia kwa karibu," alisema Kasongo.
Aidha, wakala huyo alisema anataka Samatta aende mapema kwenye klabu hiyo ili kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wake na kujitengenezea njia ya kufika mbali kisoka.
"Samatta ana miaka 24 sasa, tungependa kuona anaenda Ulaya mapema na kuonyesha uwezo wake ili akifikisha miaka 25 awe amepata njia ya mfanikio zaidi ya haya," alisema zaidi Kasongo.
Imeelezwa kuwa Genk wapo tayari kutoa kwa mabingwa hao wa Afrika kiasi cha euro milioni 2.5 (Sh. bilioni 5.9).
Katika hatua nyingine, Kasongo ameeleza kuwa ripoti ya awali ya wachezaji Haruna Chanongo na Abu Ubwa waliokuwa wakifanya majaribio TP Mazembe inaonyesha "wamefanya kweli".
"Rais wa timu (Katumbi) alikuwa nje ya nchi yake kwa hiyo walikuwa wanamsubiri ili kukamilisha kila kitu, lakini taarifa rasmi itatolewa na Stand United," alisema.
Chanongo na Ubwa wachezaji ambao ni mali ya Stand United, walikwenda kufanya majaribio ya siku 10 kwenye klabu hiyo inayoitumikia pia Mtanzania Thomas Ulimwengu.

Habari Kubwa