Mchezaji 'ala' nyekundu 2, njano 2 mechi moja VPL

22Jan 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Mchezaji 'ala' nyekundu 2, njano 2 mechi moja VPL

AJALI kazini! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mwamuzi wa kati, Amaan Simba kumuonya kwa kadi ya njano mara mbili na kumuonyesha kadi nyekundu mara mbili mchezaji mmoja katika mechi moja.

Beki kutoka Ivory Coast, Assouman N'guesemo wa Stand United ameweka rekodi hiyo mpya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya juzi kushindwa kucheza dakika zote 90 za mechi yao ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Katika dakika ya 80 ya mchezo huo ambao Stand United walipoteana kipindi cha pili, refa huyo kutoka mkoani Kagera alimlima kadi nyekundu kwa bahati mbaya mchezaji huyo jambo ambalo liliibua mvutano kidogo kabla ya refa huyo kubaini makosa yake na kuifuta kadi hiyo.
Hata hivyo, mwamuzi huyo hakuishia kuifuta kadi nyekundu, bali alimwonya kwa kadi ya njano, lakini akasahau kwamba ilikuwa kadi ya pili ya njano kwa mchezaji huyo kwani kipindi cha kwanza ambacho Stand walipata mabao mawili alikuwa miongoni mwa nyota walioonywa kwa kadi.
Ilichukua dakika tatu wasaidizi wa refa huyo kubaini kwamba N'guesemo alikuwa anacheza mechi hiyo ya kufunga mzunguko wa kwanza msimu huu akiwa na kadi mbili za njano na kumweleza Simba ambaye alimtoa kwa kumwonyesha kadi nyekundu kwa mara ya pili. Ama kweli ajali kazini!
Sheria Na. 12 ya soka (Rafu na Tabia Mbaya) na Sheria Na. 3 ya mchezo huo (Idadi ya Wachezaji) zinaweka wazi kuwa mchezaji mwenye kadi mbili za njano au aliyeonyeshwa kadi nyekundu katika mechi moja, haruhusiwi kuendelea kuwamo uwanjani.

Habari Kubwa