Mexime: Mapinduzi linabaki nchini leo

13Jan 2016
Lete Raha
Mexime: Mapinduzi linabaki nchini leo

KOCHA wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime, amesema ana matumaini makubwa ya kulibakisha nchini Kombe la Mapinduzi wakati watakapowavaa URA ya Uganda katika fainali kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa leo usiku.

Timu ya Mtibwa Sugar

Itakuwa ni fainali ya tano kwa Mtibwa katika michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya 10 na licha ya kulitwaa taji hilo mara moja tu 2010, Mexime anaamini mara hii bahati iko kwao.
"Tutahakikisha tunashinda mechi yetu ya fainali, niliweza kupambana na Simba, Yanga na Azam ambazo ni klabu kubwa hapa Tanzania kwanini nishindwe kuifunga URA ambao ni wageni?," alisema nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
“Kikosi changu kimekuwa na ubora mzuri na ndiyo maana tumetinga fainali, naamini kila kitu kitaenda sawa na mpaka sasa kikosi changu kipo tayari kwa mechi ya fainali."
Mtibwa inaingia katika fainali leo kifua mbele baada ya kuwatoa mabingwa watetezi, Simba, ambao walikutana nao katika fainali ya mwaka jana.
Miamba hao kutoka Manungu, Turiani ambao wametinga fainali kufuatia kuitoa Simba kwa bao 1-0 kwenye nusu-fainali Jumapili, wana mtihani mgumu leo dhidi ya URA iliyoruka vizingiti vyote dhidi ya Yanga kwa kusawazisha bao katika dakika za mwishoni na katika sare ya 1-1 kabla ya kuwang'oa mabingwa hao wa Tanzania Bara kwa penalti 4-3.
Kocha wa URA, Kefa Kisala, alisema kuwa anatambua ugumu wa mechi hiyo, lakini ameweka wazi kwamba hawakuja Tanzania kwa kushiriki, bali kutwaa ubingwa.
“Hatukuja kuwa washiriki tu, tumekuja kupambana na kupeleka kombe kwetu Uganda. Naamini mashabiki wetu wanangoja ushindi wetu kwa hamu hivyo tutahakikisha tunapata ushindi,” alisema kocha huyo wa timu pekee mwalikwa katika michuano hiyo mwaka huu.
Fainali iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kati ya Simba na Yanga iliota mbawa kufuatia vipigo hivyo katika mechi za nusu-fainali na hivyo kufuta uwezekano wa mahasimu hao wa jadi kukutana kwa sababu hamna mechi ya mshindi wa tatu, kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya michuano.
Yanga ilitangulia kuondoka juzi kurejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakati Simba imebaki kambini Zanzibar.

Habari Kubwa