Ajibu, Miraji wafunguka kubeba kombe Ligi Kuu

30Jun 2020
Somoe Ng'itu
Mbeya
Nipashe
Ajibu, Miraji wafunguka kubeba kombe Ligi Kuu

WACHEZAJI Ibrahim Ajibu na Miraji Athumani 'Sheva' wamefurahi kunyakua taji la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na Simba maarufu Wekundu wa Msimbazi.

Miraji Athumani 'Sheva':PICHA NA MTANDAO

Nyota hao walianza kucheza kandanda katika klabu hiyo kwenye timu ya vijana (Simba B), na baadaye kuondoka, Ajibu akisajiliwa kwa watani zao, Yanga huku Sheva akienda kuitumikia Lipuli FC ya mkoani Iringa.

Akizungumza na gazeti hili baada ya kumalizika kwa mechi kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Simba, Ajibu, alisema anamshukuru Mungu kwa kufanikiwa kushinda taji hilo msimu huu baada ya kurudi "nyumbani".

Ajibu alisema Simba ndio timu iliyomkuza katika mchezo huo, na mafanikio ambayo ameyapata msimu huu akiwa na klabu hiyo kwake ni faraja kubwa.

"Niliondoka kwa heshima na nimerudi kwa heshima mahali nilipokuzwa, nimefanikiwa kutimiza ndoto zangu kwa kutwaa taji la heshima la Ligi Kuu, asanteni mashabiki wa Simba, Simba Nguvu Moja," alisema Ajibu.

Sheva alisema ndoto yake kubwa ilikuwa kushinda taji hilo na baada ya kurejea Msimbazi aliamini ndoto zake zitatimia.

Mshambuliaji huyo alisema baada ya kutwaa taji hilo sasa akili yao ni kukamilisha mechi za ligi zilizopakia kwa mafanikio na baadaye kuhamishia nguvu kwenye michuano ya kimataifa.

"Ni jambo la furaha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, ilikuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu, niliamini itatimia msimu huu baada ya kurejea Simba, tunawashukuru wote tuliopambana tangu mwanzo wa msimu," alisema Sheva.

Simba ilifanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara juzi baada ya kufikisha pointi 79, ambazo hazifikiwi na timu nyingine, ambazo kila moja imebakiza mechi sita mkononi.

Habari Kubwa