Ajibu: Tutaendelea kuwashangaza Bara

07Dec 2018
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Ajibu: Tutaendelea kuwashangaza Bara

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Ibrahim Ajibu, amesema kuwa licha ya timu yao kutopewa nafasi ya kufanya vizuri msimu huu kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili, wamejipanga kuendelea kuwashangaza wale waliokuwa 'wanawabeza' kwa kupata matokeo mazuri uwanjani.

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Ibrahim Ajibu, picha na mtandao

Ajibu aliliambia gazeti hili kuwa wataendelea kupambana uwanjani, ili kuhakikisha wanashinda michezo yao yote ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa msimu huu.

“Walitudharau, lakini sasa tunawashangaza kwa matokeo yetu, tutaendelea kupambana uwanjani kuhakikisha hatupotezi mchezo wowote wa ligi,” alisema Ajibu.

Mshambuliaji huyo alisema pia kocha wao, Mwinyi Zahera, amekuwa akiwahamasiaha uwanjani na hata kwenye mazoezi kwa kuwataka kupambana bila kujali changamoto zilizopo.

“Ushindi wetu unaanzia kwa kocha wetu, amekuwa akituhamasisha tufanye vizuri, pia tunajitahidi kushika mbinu zake ambazo zinatusaidia kupata ushindi,” alisema Ajibu.

Aliongeza kuwa ligi ni ngumu na kila timu inataka ushindi katika mechi zake, hivyo wanafanya kazi ya ziada kujituma ili kupata ushindi. Yanga mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20, ikiwa imecheza michezo 14 na kushindi michezo 12, huku ikitoka sare mara mbili.

Kikosi hicho cha Kocha Zahera, kitakachowakaribisha Biashara United keshokutwa, ndiyo kinaongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Azam wanaoshika nafasi ya pili, huku ikiwaacha Simba kwa pointi 11 ingawa mabingwa hao wana michezo miwili mkononi.

Habari Kubwa