Bulembo ataka kigezo cha elimu Urais wa TFF kiondolewe

29May 2021
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Bulembo ataka kigezo cha elimu Urais wa TFF kiondolewe

MDAU wa Michezo nchini ,Abdallah Bulembo ameitaka Wizara ya Michezo na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kubadili Katiba na kuondoa kigezo cha elimu katika kugombea nafasi ya Urais wa Shirikisho hilo ili kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali wenye uzoefu na mpira wa miguu kugombea nafasi hiyo.

MDAU wa Michezo nchini ,Abdallah Bulembo akionesha kwa waandishi wa habari barua aliyoiandika kwa Wizara ya Michezo na TFF.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Bulembo amedai kipengele cha Katiba ya TFF kinachoweka elimu ya kiwango cha Shahada (Degree) katika kuwania Urais wa Shirikisho hilo ni kikwazo kwa maendeleo ya shirikisho kwa kuwa wapo vijana wengi wenye uzoefu na mpira ikiwemo waliowahi kuwa wachezaji na kufanya vizuri katika Soka wanaokosa fursa ya kugombea.

“Mpira huu tukiwaleta wale ambao wamehangaika na mpira ,tukipeleka shida kuhusu mambo ya mpira itatatuliwa kirahisi si imeisha mkuta ,ana historia nayo ?tukiwaruhusu hawa waliocheza mpira, waliochezesha mpira, walioumia na mpira wakaenda kuongoza mpira watafanya vizuri” amesema Bulembo .

“Ndani ya Fifa (Shirikisho la mpira wa miguu duniani) sifa za viongozi hazihitaji uwe na degree (shahada) ndani ya CAF (Shirikisho la mpira wa miguu Afrika) hakuhitajiki degree ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sifa ya kuwa Kiongozi ni kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza ndiyo sifa ya mtu aliyeko bungeni  lakini TFF lazima uwe na shahada” amesema.

Bulembo amesema ameshaiandikia barua Wizara ya Michezo na Utamaduni  kutaka kubadilishwa kwa kipengele hicho ambayo aliisoma mbele ya waandishi wa habari ambayo imenakiliwa kwa TFF na baraza la michezo nchini huku akitishia kuchukua hatua zaidi ikiwemo kwenda  Mahakamani  iwapo hatua za kubadilisha kipengele hicho hazitachukuliwa kwa kile alichodai kinakiuka Katiba ya nchi na FIFA.

“Tarehe saba mwezi wa tano nilimwandikia barua Waziri wa Michezo na Utamaduni , barua ya kwamba amuambie msajili na TFF warekebishe Katiba yao kabla hawajaenda kwenye uchaguzi kwa  sababu katiba yao inakiuka Katiba ya nchi ,Katiba ya FIFA na Katiba ya CAF” amesema Bulembo.

Amesema kwa uzoefu wake katika mpira wachezaji wengi hawana elimu ya kiwango cha shahada lakini ndiyo wanaofanya vizuri katika michezo na kutaka kama wameweza kucheza vizuri na kuiletea nchi sifa basi wapewe pia nafasi katika uongozi bila kuwekewa  vikwazo.

Habari Kubwa