Kagere kubadili mfumo Simba

21May 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Kagere kubadili mfumo Simba

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ya jijini Dar es Salaam huenda wakalazimika kubadilisha mfumo wa kucheza katika kikosi chake kama mshambuliaji wake kinara, Meddie Kagere atachelewa kuungana na wenzake wakati ligi hiyo itakaporejea tena.

MSHAMBULIAJI WA SIMBA,MEDDIE KAGERE:PICHA NA MTANDAO

Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ligi nyingine ikiwamo mashindano ya Kombe la FA yanatarajiwa kurejea tena hivi karibuni baada ya Rais John Pombe Magufuli kufiria kurejesha michezo nchini.

Mbali na Kagere ambaye alirejea kwao Rwanda, wachezaji wengine wa Simba ambao hawako nchini ni pamoja na Clatous Chama, Francis Kahata na Sharaf Shiboub.

Akizungumza na Nipashe jijini jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema benchi la ufundi la timu hiyo litapanga mfumo kwa kuzingatia wachezaji ambao watakuwa wako tayari kwenye kikosi.

Matola alisema ni mapema kuweka wazi aina ya mfumo utakaotumika mpaka pale wachezaji wao wote watakaporipoti kambini baada ya kurusa ya kufanya mazoezi pamoja itakapotolewa.

"Tusubiri wachezaji wote warudi kwanza, baada ya hapo ndio tutaangalia nani yupo na nani hayupo, Kocha Mkuu, Sven Vandanbroeck ataweza kubadili mfumo kwa kuangalia wachezaji tuliokuwa nao kwa kipindi hicho," alisema Matola.

Kocha huyo alisema wachezaji wote wanaendelea na mazoezi kwa sababu wanataka kuona wanamalizika vizuri msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Tuko tayari, tunawasubiri nyota wetu warejee, hapa kilichobakia ni kusubiri tamko rasmi la TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), ambayo itapokea rasmi ruhusa kutoka katika mamlaka husika juu za nchi," alisema Matola.

Aliongeza pia Simba iko tayari kupokea uamuzi utakaochukuliwa na shirikisho hilo kuhusu mtindo utakaotumika kumalizia ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hadi Ligi Kuu Bara inasimama kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19), Kagere ndio kinara wa kupachika mabao akiwa amefunga mabao 19.

Simba yenye pointi 71, imebakiza michezo 10 ili imalize msimu na tayari imesharudiana na wapinzani wake kwenye vita ya ubingwa ambao ni Yanga na Azam FC.

Habari Kubwa