Kocha Yanga SC avurugwa Ubelgiji

04Jun 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kocha Yanga SC avurugwa Ubelgiji

SAKATA la Kocha wa Mbelgiji wa Yanga, Luc Eymael kushindwa kurejea nchini, limeendelea kuchukua sura mpya, baada ya kubainika kuwa kuna watu 'wasiojulikana' walimvuruga kwa kutumia ujumbe kuwa klabu yake ina mpango wa kumtema ndiyo maana hawajamtumia tiketi ya ndege.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael:PICHA NA MTANDAO

Hayo yamebainishwa jana na Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alipoongea na Nipashe,juu ya maneno aliyoyatoa kocha huyo akiwa nchini kwao kuwa anakerwa na tabia ya viongozi wa klabu hiyo ya kumcheleweshea tiketi na haelewi nini kinaendelea.

Bumbuli alisema kuwa kocha wao aliongea maneno hayo kwa presha, kwani kuna watu walimpelekea taarifa kuwa kuna mpango wa kumsitishia mkataba wake, wakimueleza  kama Yanga wangetaka arejee wangeweza kufanya hivyo mapema kwa sababu makocha wenzake wote wa kigeni tayari wamesharejea nchini kuendelea na kazi.

"Tumemtuliza na yeye ametuletea meseji za watu ambao walikuwa wakimpelekea na ndizo zilizosababisha aongee maneno hayo. Kila kocha anatoka kwenye nchi yake na kila moja ilikuwa na taratibu zake za kukabiliana na corona, na si wote wanatoka Ubelgiji, lakini ukweli ni kwamba yote yamekwisha na mambo yakienda vizuri tarehe sita  atakuwa ameshawasili nchini," alisema Bumbuli.

Akijibu shutuma hizo, Afisa Habari huyo alisema kuwa awali kabisa kocha wao alikuwa na tiketi ya kwenda kwao Ubelgiji na kurudi, lakini kutokana na dunia nzima kukumbwa na ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, safari zilifutwa.

"Mwezi Aprili pia tulilipa dola 8,000 kwa ajili ya tiketi, lakini anga bado zilikuwa hazijafunguliwa na ilipofika Juni Mosi, tulianza mchakato wa kumtumia tena tiketi, lakini ikumbukwe ndiyo wakati ambapo safari nyingi za ndege zilikuwa zinaanza na anga kufunguliwa kulikuwa na safari nyingi, hivyo siku tatu nzima za mwanzo ndege zilikuwa zimejaa, ilibidi tufanikiwe kukamilisha tiketi za kuanzia tarehe nne," alisema msemaji huyo.

Habari Kubwa