Kocha Azam FC aiwahi Simba Dar

03Jun 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kocha Azam FC aiwahi Simba Dar

HATIMAYE Kocha Mkuu wa Klabu ya Azam FC, Mromania Aristica Cioaba, amerejea nchini kuendelea na kibarua chake cha kuifundisha timu hiyo kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, huku pia akiiwahi mechi ya robo fainali ya Kombe la FA, kati ya timu yake dhidi ya Simba, hapo Juni 27, mwaka huu.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Mromania Aristica Cioaba (kushoto) na Kocha wa viungo wa timu hiyo, Costel Birsan, walipowasili jijini Dar es Salaam juzi, tayari kujiandaa kwa mechi za Ligi Kuu na Kombe la FA. MPIGAPICHA WETU

Kwa mujibu wa mtandao rasmi wa Klabu ya Azam FC, Cioaba aliwasili nchini Jumatatu jioni akitokea kwao Romania alikokwenda baada ya kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19 duniani, unaosababishwa na virusi vya corona.

Kocha huyo aliwasili pamoja na kocha wa viungo, Costel Birsan, wakitokea Frankfurt, Ujerumani ambako ndiko walikopata usafiri wa ndege ya kurejea Tanzania.

Makocha hao walikwama kurejea ndani ya muda kutokana na nchini kwao kuwapo kwa karantini ya ugonjwa huo.

Taarifa ya Azam imeeleza kuwa wawili hao walitarajia kuanza kazi jana jioni, huku kikosi hicho kikiwa tayari kilishaanza mazoezi Jumatano iliyopita chini ya Kocha Msaidizi, Mrundi Bahati Vivier.

Azam itakuwa na kibarua cha Ligi Kuu Juni 14, mwaka huu itakapocheza kwenye uwanja wao wa nyumbani, Azam Complex dhidi ya Mbao FC kutoka Mwanza.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael, anatarajiwa kuwasili nchini wiki akitokea nchini kwao Ubelgiji.

Kocha huyo naye alikwama kutokana na karantini ya ugonjwa wa corona nchini kwao, na kwa sasa mazoezi yanasimamiwa na Boniface Mkwasa.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, amesema utaratibu wote umeshafanyika na huenda wakawa naye wiki hii, hata wakasafiri naye mjini Shinyanga ambako Yanga inakwenda kucheza dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage mjini huko.

"Unajua usafiri kwa sasa si rahisi hivyo, anatoka kwao, anapitia Ujerumani ambako ndiko kuna usafiri wa kwenda Ethiopia, ndiyo aje Dar, husafiri tu hivi hivi, lakini ndani ya wiki hii tunatarajia atakuwa nchini na hata safari ya kwenda Shinyanga huenda tukawa naye," alisema Bumbuli.

Yanga itacheza mechi hiyo dhidi ya Mwadui Juni 13, mwaka huu.

Habari Kubwa