Matumla, Ustadhi waeleza mabondia wanapoteleza

07Apr 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Matumla, Ustadhi waeleza mabondia wanapoteleza

BONDIA mkongwe nchini, Rashid Matumla " Snake Boy", amesema mchezo huo unapoteza umaarufu kutokana na mabondia chipukizi kukosa msingi mzuri wa maandalizi kuanzia ngazi za chini.

BONDIA mkongwe nchini, Rashid Matumla " Snake Boy", picha mtandao

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Matumla alisema kutokana na kukosekana mfumo sahihi, hali hiyo huwafanya mabondia chipukizi "kukurupuka" kujiunga na ngumi za kulipwa hali ya kuwa hawajapata uzoefu hivyo kuishia kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa wanayoshiriki ndani na nje ya Tanzania.

"Mimi ninashauri ili kuwabana mabondia kujiunga na ngumi za kulipwa wakiwa hawana uzoefu wa kutosha, ni lazima zitolewe leseni maalumu, hii itasaidia kuwajenga na kutangaza vizuri jina la Tanzania," alisema Matumla.

Aliongeza kuwa siri ya familia yao kufanya vizuri katika mchezo huo ni kujituma kwenye mazoezi ambayo yalisimamiwa kwa kiwango kikubwa na baba yao mzazi ambaye sasa ni marehemu.

Bondia huyo wa zamani wa dunia, alisema pia pambano lake la kwanza dhidi ya Francis Cheka liliandaliwa baada ya bondia huyo kutoka Morogoro kumfuata nyumbani kwao Keko kumuomba wacheze.

"Cheka alifanikiwa kunipiga katika pambana la Morogoro baada ya kuanza kuumwa mgongo, ndio walipoanza kutoka madogo, Cheka alinipiga, Maugo (Mada), ilikuwa njia yao kupata majina," alisema Matumla.

Aliongeza sababu kuu iliyomfanya kuondoka kwa aliyekuwa promota wa ngumu, Jamal Malinzi na kujiunga na Alex Kajumulo, ni kukaa muda mrefu bila ya kutetea mikanda aliyokuwa anaishikilia.

Naye promota wa ngumi maarufu nchini, Yassin Abdallah "Ustadhi", alisema ili kupata mabondia wenye uwezo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, ni mabondia husika kukubali kuanzia kwenye ngumi za ridhaa kwanza.

Ustadhi alisema mabondia wanapokimbilia kucheza ngumi za kulipwa hali ya kuwa hawajapata uzoefu, wanashindwa kung'ara na wachache ndio hufanya vizuri.

Alishauri serikali kuweka sheria za kuwabana mabondia kufuata misingi kabla ya kujiunga na ngumi za kulipwa kwa sababu mapromota hawana muda wa kuwaendeleza zaidi ya kufikiria maslahi yao binafsi.