Morrison, Tshishimbi waitia hofu Yanga

03Jun 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Morrison, Tshishimbi waitia hofu Yanga

WAKATI Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael, akitarajiwa kurejea nchini wakati wowote wiki hii, msaidizi wake, Boniface Mkwasa amesema wachezaji nyota wa timu hiyo winga mshambuliaji Bernard Morrison na kiungo mkabaji Papy Tshishimbi, wameitia hofu timu hiyo baada ya kupata maumivu.

Mkwasa, jana aliwaambia waandishi wetu kuwa nyota hao wameonekana kuwa na majeraha na wanaendelea kuwaangalia kwa karibu.

"Si majeraha makubwa, tunaamini mpaka kufika Juni 13, watakuwa fiti na kusafiri nao kwenda Shinyanga kwenye mchezo wetu wa kwanza," alisema Mkwasa.

Kuhusu mchezo wao huo ambao utakuwa dhidi ya Mwadui FC, Mkwasa alisema wamejipanga kikamilifu kuelekea katika mchezo huo, licha ya kwamba wanatambua kucheza ugenini kuna changamoto zake.

Mkwasa alisema anashukuru wachezaji wote walioripoti kambini wanaendelea vizuri isipokuwa hao wawili ambao wamepata maumivu kidogo mazoezini.

"Tumejipanga vizuri kukutana na Mwadui hatuibezi ni timu nzuri lengo letu ni kurudi na pointi tatu nyumbani," alisema Mkwasa.

Wakati huo huo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli, aliliambia Nipashe kuwa Kocha Mkuu, Eymael anatarajia kurejea nchini wakati wowote wiki hii kuendelea na majukumu yake.

Habari Kubwa