Niyonzima kimeeleweka Yanga

19Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Niyonzima kimeeleweka Yanga
  • ***Dk Msolla amwachia mpini Zahera aamue moja kabla ya kumwaga wino rasmi, lakini...

HATIMAYE Kiungo fundi mwenye pasi nyingi za kufika, Mnyarwanda Haruna Niyonzima, sasa ni muda tu unasubiriwa kufika na Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera kuamua moja kabla ya kurejea rasmi kuitumikia klabu hiyo ya Mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Niyonzima aliyeibukia Rayon Sports na kuichezea kuanzia mwaka 2006–2007 kabla ya kutua APR mwaka 2007–2011 kisha kujiunga na Yanga kuanzia 2011–2017, kwa sasa anaitumikia A.S Kigali ambayo alijiunga nayo akitoka kuitumikia Simba alipodumu kuanzia mwaka 2017–2019.

Baada ya taarifa kuzagaa kuwa kiungo huyo wa kimataifa wa Rwanda anataka kurejea kuitumikia Yanga, hatimaye uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani jijini Dar es Salaam umethibitisha rasmi.

Akizungumza na mwandishi wetu, juzi, Mwenyekiti wa Yanga, Dk. Mshindo Msolla, alisema ni kweli ameonana na kuzungumza na Niyonzima ambaye ameeleza nia yake ya kurejea kwa mara nyingine kuitumikia klabu yao.

"Ni kweli nilipokuwa Rwanda kikazi wiki iliyopita nilimpigia simu Niyonzima nikamueleza hoteli nilipo kwa lengo tu la kutaka kuonana naye kumsalimia, hata hivyo aliniambia mwalimu tayari nimekusoma kwenye mitandao najua upo hapa,". "Alipofika tulizungumza na kunieleza yupo tayari kurudi Yanga," alisema Dk. Msolla.

Alisema hawezi kutolea uamuzi suala hilo kwa kuwa hilo ni jukumu la Kocha Mkuu, Zahera kutazama mchezaji anayemhitaji na kama akiona Niyonzima ana nafasi katika kikosi chake basi watafanya mchakato wa kumsajili.

"Tusubiri dirisha dogo lifunguliwe, endapo kocha atahitaji kuboresha kikosi chake na kuamua kama Niyonzima anamhitaji hapo ndipo tunaweza kufanya uamuzi," alisema Dk. Msolla.

Yanga kwa sasa ipo jijini Mwanza ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC Jumanne wiki hii kabla ya kuikaribisha Pyramids ya Misri kwenye mchezo wa mchujo kuwania kushiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga iliyoangukia hatua hiyo baada ya kutolewa raundi ya kwanza na Zesco United kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, itaikaribisha Pyramids Jumamosi ijayo Oktoba 27 kabla ya kurudiana wiki mbili zijazo nchini Misri.