Pongezi Waziri Mkuu, mashabiki Simba SC

14Jan 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Pongezi Waziri Mkuu, mashabiki Simba SC

WAWAKILISHI wa Afrika Mashariki na Kati katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ya jijini Dar es Salaam, wameanza vema hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao 3-0 nyumbani.

Kwa ushindi huo walioupata katika Uwanja wa Taifa dhidi ya JS Saoura ya Algeria juzi, unaifanya Simba kukaa kileleni mwa Kundi D. Hiyo ni kutokana na Al Ahly ya Misri nayo ikiwa nyumbani juzi kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa ujumla tunaipongeza Simba kwa kutumia vema faida ya kucheza uwanja wake wa nyumbani ikiungwa mkono na mashabiki wake na Watanzania kwa ujumla. Mbali na ushindi wa juzi, Nipashe imefurahishwa zaidi na namna maelfu ya mashabiki na Watanzania kwa ujumla walivyojitokeza kuipa sapoti Simba.

Tunatambua mashabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani, na kwa namna wapenzi wa Simba, mashabiki, wadau wa soka na Watanzania kwa ujumla walivyojitokeza kwa wingi, tunaamini wamechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa ushindi huo.

Aidha, tunachukua nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, kwa kujaliwa kwake kupenda soka na kuwa mstari wa mbele kwenda kuipa sapoti Simba kwenye Uwanja wa Taifa juzi.

Hakuna aliyetarajia kumuona Waziri Mkuu uwanjani hapo hasa kutokana na majukumu makubwa yaliyokuwa yakimkabili siku hiyo ya kuadhimisha Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Kisiwani Pemba.

Majaliwa alikuwa miongoni mwa waheshimiwa waliohudhuria mahadhimisho hayo, lakini kwa kuonyesha unamichezo wake baada ya sherehe hizo alifunga safari na kuuwahi mchezo huo wa Simba.

Kadhalika, pamoja na viongozi wengine lakini pia tunampongeza Mgeni Rasmi Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson kwa kuwa miongoni mwa waliokuwa wakiwasapoti wawakilisha hao pekee wa nchi kimataifa.

Ni wazi uwapo wao uwanjani hapo ulichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wa Simba, kwa kuwa wachezaji walihamasika kuwa pamoja na serikali na hawakutaka kuwaangusha.

Tunaomba ushirikiano ulioonyeshwa kuanzia kwa mashabiki hadi viongozi wa vyama vya siasa na serikali uendelee kwa mechi zote za wawakilishi hao wa nchi kimataifa.

Tunatangulia kuweka wazi kwamba Nipashe ni gazeti huru halina klabu, lakini linapokuja suala la uzalendo hususan ni kwa wawakilishi wa nchi katika michuano ya kimataifa, litaendelea kuwa mstari wa mbele kuunga jitihada zao katika kupeperusha bendera ya nchi.

Kwa mantiki hiyo, wakati huu Simba ikijiandaa kwa mechi yao ya pili ugenini dhidi ya AS Vita, tunawaomba mashabiki, wanachama wa klabu hiyo, wadau wa soka, viongozi wa vyama na serikali na Watanzania kwa ujumla kuungana pamoja kwenda kuipa sapoti kama ilivyokuwa Uwanja wa Taifa juzi.

Tunaamini kama robo tu ya maelfu ya mashabiki wa Simba na Watanzania kwa ujumla waliojitokeza juzi, wataungana na Simba kwenda DR Congo kwa ajili ya mechi yao ya Jumamosi, hakuna kitakachoizuia kuendeleza ushindi.

DR Congo si mbali, hivyo ni wakati sasa wa kutambua thamani na heshima ya Klabu ya Simba inayopeperusha bendera ya nchi kwa kwenda kuiunga mkono ugenini.

Tunaitakia Simba maandalizi mema kuelekea mchezo huo wa Jumamosi na mingine inayofuata ya kimataifa ukiwamo wa Februari 2, mwaka huu dhidi ya Al Ahily ugenini.