RC- Kaitaba itakuwa machinjio ya timu za Ligi Kuu

06Sep 2020
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe Jumapili
RC- Kaitaba itakuwa machinjio ya timu za Ligi Kuu

MKUU wa mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amezitaka timu za Ligi Kuu Tanzania Bara zitakazokwenda kucheza na timu ya Kagera Sugar katika uwaja wa Kaitaba zijiandae, maana hazitatoka salama katika uwanja huo, kutokana na kikosi cha timu hiyo kuwa imara zaidi.

Akizungumza wakati wa kukitambulisha rasmi kikosi cha timu ya Kagera Sugar, Gaguti alitangaza uwanjwa wa Kaitaba kuwa machinjio ya timu zote zitakazofika mkoani Kagera kucheza na timu hiyo.

"Tumedhamiria msimu huu, lazima tuwe mabingwa wa ligi kuu ya Vodacom, tumefanya maandalizi mazuri katika nyanja zote za kikosi na usafirishaji, ili wachezaji wetu wasafiri kwa raha," alisema.

Aidha alitoa ofa kwa mashabiki wa timu ya Kagera Sugar kuingia uwanjani bure katika mechi ya kwanza na ya tatu.

"Natoa ofa, mechi ya kwanza mashabiki 500 wataingia bure, mechi ya pili mashabiki 500 nao wataingia bure, lakini pia mechi ya tatu mashabiki 500 wataingia bure lengo kutia hamasa timu yetu," alisema.

Mwenyekiti wa chama cha soka mkoa Salumu Umande Chama aliwataka mashabiki wa Kagera Sugar kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao na kuwa shabiki ni nguzo ya ushindi.

Chama alisema Kagera Sugar itakuwa na mchezo wa kwanza ambao itacheza na JKT Septemba 07, mchezo wa pili itacheza na timu ya Yanga Septemba 19 na itakuwa na mchezo wa tatu na KMC Septemba 25.

Naye msemaji wa kiwanda cha sukari cha Kagera Vincent Mtaki alisema kuwa wanaitegemea timu ya Kagera Sugar kufanya vizuri katika msimu huu kutokana na maboresho ya kikosi yaliyofanyika.

Kocha mkuu wa Kagera Sugar Meck Mexime alisema kikosi chake kiko vizuri na kuwa wamecheza mechi za kirafiki na timu mbalimbali ikiwamo KMC, Mtibwa Sugar na Mwadui FC.

Kutambulishwa kikosi cha Kagera Sugar kumekwenda sambamba na kuchezwa kwa mechi ya kirafiki baina ya Kagera Sugar na Kagera Combine ambapo hadi dakika 90 zinamalizika, Kagera Sugar iliibuka na ushindi wa mabao manne kwa moja.

Habari Kubwa