Samatta aelezea avyoitungua City

03Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Samatta aelezea avyoitungua City

BAADA ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kuungana na nyota wengine wanne wa Afrika waliowahi kufunga kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Ligi nchini England (EFL Cup), hatimaye amefunguka alivyowatungua wapinzani wao, Manchester City.

Samatta amekuwa mchezaji wa tano Afrika kufunga katika mechi ya fainali ya EFL akiungana na Didier Drogba (aliyefunga manne), Joseph-Desire Job, Obafemi Martins na Yaya Toure.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Wembley juzi, Samatta alifunga bao hilo dakika ya 41 kwa kichwa akiunganisha kimyani krosi iliyochongwa kutoka wingi wa kushoto na Anwar El Ghazi wakati wakiwa nyuma kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Sergio Aguero na Rodri dakika ya 20 na 30.

Akizungumzia na mwandishi wetu, Samatta alisema walijua mechi itakuwa ngumu kutokana na ubora wa Manchester City, lakini waliingia dimbani kwa lengo la kupambana kupata matokeo, hata hivyo haikuwa bahati yao. Kuhusu alivyofunga bao hilo, Samatta alisema:

"Wakati mpira unapigwa [na Anwar El Ghazi] ulikuja nadhani nyuma ya Fernandinho [beki wa Man City] na alishakata tamaa kurudi kuuwahi, hivyo nilichokuwa nafikiri ni kuuweka sehemu sahihi."

Kwa ushindi huo unaifanya Manchester City kutwaa kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo, lakini likiwa mara ya nne kwao katika misimu mitano.

Habari Kubwa