Simba kutangazia ubingwa Nangwanda

04Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba kutangazia ubingwa Nangwanda
  • Sven ageukia utimamu wa mwili, asema siku 10 zilizobaki zinatosha nyota wake kuanza...

HUKU Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck, akieleza kuwa ameisoma ratiba ya Ligi Kuu, lakini wachezaji wake hawajawa tayari kwa upande wa utimamu wa mwili, hesabu zinaonyesha mabingwa watetezi hao wanaweza kutangazia ubingwa wao wakiwa ugenini .

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck:PICHA NA MTANDAO

Kwa sasa zimebaki siku 10 kabla ya Simba kucheza mechi yake ya kwanza tangu Ligi Kuu Bara iliposimama Machi 17, mwaka huu kutokana na mlipuko wa maambukizo ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu, COVID-19.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa Jumatatu wiki hii na Bodi ya Ligi (TPLB), Simba itacheza mechi yake ya kwanza katika Uwanja wa Taifa dhidi ya Ruvu Shooting Juni 14 ikiwa ni siku moja baada ya watani zao, Yanga kuvaana na Mwadui FC katika dimba la Kambarage mkoani Shinyanga.

Na baada ya mechi hiyo, Simba ambayo ina pointi 71 huku ikihitaji alama 14 tu ili kutangazwa mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo, Juni 20 itaialika Mwadui FC katika Uwanja wa Taifa kabla ya siku nne baadaye kuivaa Mbeya City katika dimba la Kumbukumbu ya Sokoine na kisha Julai Mosi kuivaa Tanzania Prisons kwenye uwanja huo.

Kama itavuna pointi hizo 12 katika michezo hiyo minne, Julai 5, mwaka huu itaifuata Ndanda FC ikiwa na lengo moja tu la kutangazia ubingwa Mtwara, wakati itakapohitaji ushindi ili kuruhusu mashabiki wake kuanza kusherehekea ubingwa huo wakiwa Mtwara huku wakibakiza mechi tano dhidi ya Namungo FC, Mbao FC, Alliance FC, Coastal Union kabla ya kuhitimisha na Polisi Tanzania katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi hapo Julai 26, mwaka huu.

Pointi hizo 14, zinatosha kuifanya Simba kufikisha alama 85 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na Azam inayoshika nafasi ya pili kwa sasa kuwa na pointi 54 huku timu hizo kila moja ikibakiza mechi 10, hivyo ikishinda mechi zake zote itafikisha alama 84.

Hata hivyo, pamoja na kukiri wachezaji wake kutokuwa tayari, Sven amesema wiki mbili zinatosha kuwarejeshea wachezaji wake utimamu wa mwili tayari kuanza mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Sven alisema kwa sasa bado wachezaji wake hawako tayari kurejea kuanza kucheza ligi kwa sababu hawana utimamu wa mwili kutokana na kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu, lakini siku zilizobaki kabla ya kushuka dimbani, zinamtosha kuwarejesha kuwa fiti.

Alisema kinachohitajika kwa sasa ni muda zaidi wa kufanya mazoezi ya pamoja ili kurejesha utayari wa mwili, stamina na kasi kabla ya kuanza mikikimikiki ya ligi siku 10 kutoka sasa.

“Nitaendelea kubadili mifumo ya mazoezi kwa kadiri muda unavyozidi kwenda ili kuwaweka tayari wachezaji kabla ya ligi kurejea kwani tuna wiki moja tangu tulipoanza kujifua.

“Ratiba nimeiona, ukiniambia kuwa kwa sasa tupo tayari kucheza nitakwambia hapana, kwa sababu wachezaji hawana utimamu wa mwili. Kwa hizi siku zilizobaki kabla ya ligi kurejea zitatusaidia kutuweka vizuri na jambo zuri ni kwamba asilimia kubwa wachezaji wote wako kikosini isipokuwa wawili tu,” alisema Sven.

Sven aliwataja wachezaji ambao bado hawajarejea nchini na kujiunga na wenzao kikosini kuwa ni kiungo Mzambia Clatous Chama ambaye alisema atarejea Jumatatu ijayo huku wakiwa hawajui ni lini kiungo Msudan Sharaf Eldin Shaiboub atarejea kwa kuwa mipaka ya nchi yao bado imefungwa kutokana na janga la corona. 

Habari Kubwa