Simba yawazuia Okwi, Bocco kusepa

21Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yawazuia Okwi, Bocco kusepa
  • ***Salamba njiani kutimkia Ubelgiji, mazungumzo yafika pazuri...

KUTOKANA na majukumu ya kimataifa ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili, uongozi wa klabu ya Simba umezuia kuondoka kwa sasa washambuliaji wake wawili, Emmanuel Okwi na John Bocco wanaowaniwa na klabu kutoka Afrika Kusini na Misri.

Okwi, anawaniwa na klabu ya Kaizer Chief wakati Bocco anawaniwa na klabu kutoka nchini Misri ambao wamewasilisha maombi yao.

Mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo aliiambia Nipashje jana kuwa, walipokea barua ya Kaizer Chief wanayemtaka Okwi, lakini klabu hiyo imechelewa kuafikiana na Simba juu ya malipo mpaka dirisha dogo limefungwa.

Kiongozi huyo alisema walitaka wampate mbadala wa Okwi kabla ya kumwachia kwenda kwenye klabu hiyo, lakini sasa watalazimika kuwa naye kutokana na majukumu ya kushiriki michuano ya kimataifa.

“Kwa Okwi, Kaizer Chief wenyewe wamechelewesha mambo, walileta maombi na sisi tukawapa dau letu sasa wamechelewa kutupa mwelekeo kama wameafiki, kwa sasa hatuwezi kumwachia kwa sababu tupo kwenye mashindano ya kimataifa na hatujasajili mbadala wake,” alisema kiongozi huyo.

Alisema Simba haina kawaida ya kumzuia mchezaji kuondoka na kama itatokea tena timu hiyo inamuhitaji na kufikia mwafaka watamruhusu Okwi kuondoka.

Aidha, alisema sababu hizo hizokwa Okwi zimemzuia pia Bocco kuondoka kwenda Misri anapohitajika kwenye moja ya klabu inayoshiriki ligi kuu nchini humo.

“Tumepokea barua ya klabu hiyo, lakini kama ilivyo kwa Okwi, hatuwezi kuwaachia wachezaji wa kikosi cha kwanza waondoke wakati bado hatujapata mbadala wao,” alisema.

Kiongozi huyo aliongezea kuwa, kuna ofa mezani kwao kutoka Ubelgiji ambapo kuna klabu inayomuhitaji mshambuliaji wao Adam Salamba.

“Kwa Salamba mazungumzo yanaendelea, kama tutafikia mwafaka tutamruhusu kuondoka, yeye (Salamba) ana nafasi ya kwenda Ubelgiji mambo yakikamilika kila kitu kitakuwa wazi,” alisema kiongozi huyo.

Simba kwa sasa ipo kwenye maandalizi kuelekea kwenye mchezo wao wa marudiano wa ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Nkana Rangers.

Mchezo huo utachezwa Jumapili kwenye uwanja wa taifa ambapo Simba inahitaji bao moja tu kuweza kutinga hatua ya makundi, mchezo wa kwanza mabingwa hao wa Tanzania walifungwa mabao 2-1 ugenini Zambia.

Habari Kubwa