Simba, JS Saoura hatumwi mtoto

12Jan 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, JS Saoura hatumwi mtoto
  • ***Yes We Can yaandaliwa kuwamaliza Waarabu...

YES WE CAN. Hiyo ndio kauli mbiu ambayo inatumiwa na wawakilishi pekee wa mashindano ya kimataifa wa Afrika Mashariki na Kati, Simba kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura kutoka Algeria utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa Dar

Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems

Katika kujiandaa na mechi hiyo, Simba iliweka kambi Zanzibar na kutumia mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo yatamalizika kesho, kuwanoa wachezaji wake ili kuhakikisha wanapata pointi tatu katika mchezo wao wa kwanza hapa nyumbani.

Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Patrick Aussems amesema kuwa anatambua ugumu na ushindani ambao atakutana nao katika mchezo huo lakini anaamini kikosi chake kitaanza vyema hatua hiyo na kuwapa furaha mashabiki wake.

Aussems, alisema kuwa anazifahamu vyema mbinu zinazotumiwa na timu za Kiarabu, hivyo amekiandaa vizuri kikosi chake ili kupata ushindi katika mchezo huo kwa kuongeza umakini na kuweka akilini kwamba wanaweza.

"Timu nyingi za kiarabu nazitambua hasa kutokana na uzoefu nilionao, nimezifuatilia namna ambavyo wanafanya na nimegundua kuwa wachezaji wao ni wajanja sana, wanatabia ya kupiga sana kelele wakiwa uwanjani na wana mtindo wa kujiangusha angusha, hilo lipo wazi nimeligundua na nimelifanyia kazi," alisema Aussems.

Kocha huyo aliongeza kuwa benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wamejipanga kutofanya makosa katika mechi zote za nyumbani, kwa kujipanga kuvuna pointi tisa ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Kikosi cha JS Saoura kilitua nchini juzi kikiwa kinaongozwa na mshambuliaji wake Mtanzania, Thomas Ulimwengu ambaye amesajiliwa hivi karibuni akitokea Sudan.

"Tumekuja kwa ajili ya kutafuta pointi tatu, sisi tumejiandaa na Simba pia imejiandaa, timu bora itavuna matokeo mazuri," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Naibu Spika, Tulia Ackson, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mechi hiyo ya kimataifa itakayochezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Simba yenye pointi 33, inashuka katika mchezo huo ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini wana mechi tano za viporo wakati msimamo wa Ligi Kuu ya Algeria 'Ligue 1', JS Saoura ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 23.

Habari Kubwa