Simba, Namungo wakati utaongea

07Jul 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Namungo wakati utaongea
  • Kocha Sven aeleza mechi hiyo itawasafishia njia kuelekea mchezo dhidi ya watani Jumapili...

SAFISHA njia! KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema amekiandaa kikosi chake kuondoka na ushindi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuikabili Yanga.

KOCHA Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck:PICHA NA MTANDAO

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/20, Simba watakutana na Yanga katika mechi ya hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA, itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini, Dar es Salaam.

Akizungumzia na gazeti hili jana, Sven alisema anataka kuona kikosi chake kinaweka rekodi ya kucheza fainali za Kombe la FA, baada ya kuwatoa wapinzani wao wa jadi, Yanga ambao waliwafunga kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania walipokutana Machi 8, mwaka huu.

Sve alisema kwa sasa akili yao imeelekea katika kuikabili Namungo na wanatarajia kupata pointi tatu ambazo zitaongeza furaha katika sherehe za kukabidhiwa kikombe.

Alisema mchezo wa Jumatano (kesho), ni sehemu mojawapo ya kukijenga kukiimarisha kikosi chake kuelekea 'hesabu' za kuwaharibia wapinzani wao Yanga katika 'mtangange' wa Kombe la FA, hatua ya nusu fainali.

"Tupo hapa (Mtwara), kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wetu ujao dhidi ya Namungo, ikiwa pia ni maandalizi ya mchezo wa FA dhidi ya Yanga, hakuna mchezo mwepesi, wao wanahitaji matokeo na sisi pia tunahitaji matokeo mazuri, tupo kwa ajili ya kupambana na kupata matokeo mazuri na kuvuka hata ya nusu fainali, "Sven alisema.

Naye nahodha wa timu hiyo, John Bocco, alisema wako tayari na imara kuwakabili Namungo ambayo inaundwa na wachezaji wenye uzoefu na ligi hiyo.

Bocco alisema anaimani hawatawaangusha mashabiki wao ingawa wanajua wapinzani wao wana timu nzuri na yenye rekodi nzuri ikiwa nyumbani.

"Sisi kama wachezaji tupo vizuri, tutapambana tupate matokeo, tunajua Yanga ni timu nzuri, na hata Namungo, tulicheza nao mara ya kwanza tulipata matokeo, lakini haikuwa rahisi hivyo, tunajua nao wamejipanga lakini nasi tunataka tuchukue kombe huku tukiwa tumeshinda, " Alisema Bocco.                                    

Naye Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema kikosi cha timu hiyo kitaondoka Mtwara leo jioni na kuelekea Lindi tayari kwa mechi hiyo.

Rweyemamu alisema anawaomba mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi kwa sababu wanataka kukabidhi kombe la ubingwa wakiwa na furaha.

Alisema pia wanaamini beki wao, Shomary Kapombe, ambaye aliumia katika mechi dhidi ya Azam FC, atarejea mapema uwanjani.

Habari Kubwa