Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, aliliambia gazeti hili kuwa pamoja na kuwa wameshatetea ubingwa, watashuka uwanjani kuikabili Ndanda wakidhamiria kupata ushindi na si kukamilisha ratiba.
Rweyemamu alisema kila mchezo kwao ni muhimu na watashuka uwanjani wakifahamu wenyeji wao wanahitaji ushindi ili kujiondoa kwenye janga la kushuka daraja.
"Tunahitaji ushindi, tunahitaji kuupa heshima ubingwa wetu, tutacheza kwa nguvu ile ile ya mwanzoni," alisema kwa kifupi meneja huyo.
Baada ya mchezo huo, Simba itaeelekea Lindi kwa ajili ya kuwavaa Namungo FC katika mechi nyingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Kassim Majaliwa.
Mabingwa hao wanatarajia kukabidhiwa kombe baada ya kutwaa ubingwa kwa msimu wa 2019/20 na kombe hilo litakuwa ni la kwao jumla kwa sababu ya kulitwaa mara tatu mfululizo.