Sirari waomba bidhaa za nje zipunguzwe kodi

12Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Tarime
Nipashe
Sirari waomba bidhaa za nje zipunguzwe kodi

WANANCHI na wafanyabiashara wa Kata ya Sirari, wilayani Tarime mkoani Mara, wameiomba serikali kupunguza kodi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka Kenya ili kukomesha biashara ya magendo.

Wafanyabiashara hao wametaja bidhaa hizo kuwa ni pamoja na saruji, sukari na mafuta ya kula.

Wananchi hao wameiomba serikali kushusha kodi kwa bidhaa ya saruji inayotoka nchini Kenya ili iwe rafiki kwa wafanyabiashara ikizingatiwa kwamba Wilaya ya Tarime imepakana na nchi hiyo.

Wananchi hao walieleza hayo kwa Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Waitara ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), alisikiliza kero mbalimbali zinazowakabili.

Diwani wa Kata ya Sirari, Amos Sagara (CCM), alisema wananchi hawakwepi kulipa kodi, lakini kinachosababisha wapitishe bidhaa kwa njia za panya wanakwepa kodi kubwa kwa kuwa inawaumiza kibiashara.

"Wananchi hawakwepi kulipa kodi tatizo lipo serikalini wameweka kodi kubwa sana unapoingiza bidhaa za Kenya angalau saruji wangetoza hata Sh. 3,000 kwa kila mfuko. Wakikamatwa na bidhaa za Kenya wanapigwa kwa mipini ya jembe, pikipiki zimekamatwa wafanyabiashara wa bidhaa wanateseka, watu wanahitaji kupewa maelekezo, kodi za bidhaa na punguzo la malipo ya kodi kwa bidhaa zitokazo Kenya serikali ikifanya hivyo hakuna atakayekwepa kulipa kodi,” alisema Sagara.

Chacha Mwita, mkazi wa eneo hilo, alisema Kata ya Sirari imepakana na Kenya na bidhaa za nchi hiyo zina bei nafuu ikilinganishwa na za Tanzania na kuwa kitendo cha kuzizuia ni kuwaumiza wananchi wa mipakani.

"Saruji ya Tanzania mfuko mmoja unauzwa Sh. 22,000, bado usafiri na wakati mwingine upatikanaji wake ni wa shida, mpakani Kenya saruji inauzwa kwa Sh. 12, 000 hadi 13, 000, ikiingia Tarime inauzwa Sh. 17,000 na upatikanaji wake ni rahisi," alisema Chacha.

Mbunge Waitara alisema kuwa saruji imekuwa ni tatizo kubwa kwa wananchi wilayani Tarime na kutaka suala hilo liangaliwe zaidi kwa kuwa linawaumiza wananchi na kuahidi kulifikisha mamlaka husika ili litatuliwe...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa