Sven atenga saa 48 hatari

10Jul 2020
Somoe Ng'itu
Ruangwa
Nipashe
Sven atenga saa 48 hatari
  • Mbelgiji huyo aeleza wanataka kukamilisha hesabu za msimu huu kibabe, Manara atamba Jumapili hawachomoki... 

BAADA ya kukabidhiwa kikombe cha ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2019/20, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema leo ndio anaanza kupanga mikakati ya ushindi kuelekea mchezo wao wa nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Yanga utakaochezwa Jumapili .

Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck:PICHA NA MTANDAO

Akizungumza na Nipashe mjini hapa, Sven, alisema hakutaka kuufikiria mchezo huo mapema kwa sababu anaifahamu vema Yanga hivyo, safari hii wasubiri kuona makali na hasira za kikosi chake.

Sven alisema hata walipokuwa wakiwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baadhi ya wapinzani wao walikisema kikosi chake lakini mwisho wake wameshuhudia kombe likitua Msimbazi kwa msimu wa tatu mfululizo.

Mbelgiji huyo alisema mechi hiyo kwake ni rahisi kwa sababu amebakiza "hesabu" za kuwania taji hilo bila ya presha ya kuwaza tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa kama walivyo watani zao Yanga.

"Sikuwahi kuifikiria Yanga, wacha kwanza tufike Dar es Salaam, halafu ndio tuanze mikakati ya kuelekea mchezo huo wa nusu fainali, tutakuwa na siku mbili za mazoezi, zinatosha kuimarisha mipango yetu," alisema Sven.

Kocha huyo alisema atakuwa na uhuru wa kupanga kikosi chochote baada ya baadhi ya nyota wake kupumzika katika mchezo uliopita dhidi ya Namungo FC ambao ulimalizika kwa suluhu.

"Sitaki kuwaahidi mashabiki nini tutafanya, hii imebaki baina yangu na wachezaji, nitazungumza na kuwaambia wanachotakiwa kukifanya Jumapili, tusubiri," Mbelgiji huyo aliongeza.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Setho Mbatha, alisema mechi hiyo itakuwa ngumu na wamejiandaa kukabiliana na ushindani kutoka kwa watani zao.

Mbatha alisema wanajua Yanga wataingia na presha ya kutaka ushindi kujihakikishia na safari ya kuchukua kombe hilo ili washiriki mashindano ya kimataifa, huku wao wakikataa kupoteza tena dhidi ya vigogo hao.

"Itakuwa na ushindani kutoka pande zote mbili, kila timu itaingia kuhakikisha malengo yake yanafanikiwa, kwetu tumejipanga kuhakikisha haturudii makosa, kupoteza tena mchezo wa 'dabi' haiwezekani, tunahitaji kufanya nguvu ya ziada kama mabingwa," Mbatha alisema.

Aliongeza anafurahi kuona msimu wake wa kwanza wameshinda taji la Ligi Kuu Tanzania Bara na anatarajia kukamilisha furaha ndani ya klabu hiyo kwa kulipa kisasi cha kuifunga Yanga na kuiondoa kwenye kampeni ya kuwania kombe hilo la tatu msimu huu.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, Haji Manara, aliendelea kutamba timu hiyo imeshachukua makombe matatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa yamebaki saba katika mkakati wao wa kushinda mara 10 mfululizo.

Manara aliwataka watani zao Yanga pamoja na timu nyingine wasiweze mawazo ya kushinda taji hilo mpaka kuanzia mwaka 2027 ambapo wao wanaweza kuliachia.

"Kesho (jana) tutakuwa na sherehe za ubingwa, tutalikabidhi kombe letu pale klabuni, halafu tutaanza mikakati ya kuwamaliza Yanga, watatueleza walichomokaje siku ile, watatoa jibu Jumapili," Manara alitamba.

Mbali na mchezo huo, nusu fainali nyingine itakuwa kati ya Namungo FC dhidi ya timu ya Daraja la Pili, Sahare All Stars ya jijini, Tanga.

Habari Kubwa