Watani wa jadi kumaliza ubishi

25Sep 2021
WAANDISHI WETU
Dar es Salaam
Nipashe
Watani wa jadi kumaliza ubishi
  • ***Makocha wafunguka huku vikao vya 'mauaji' vikiendelea kila...

WASWAHILI wanasema usiku wa deni haukawii. Hatimaye siku ya mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga uliokuwa unazungumziwa utachezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mechi hiyo ni rasmi kwa ajili ya kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22.

Inaweza ikawa mechi ngumu zaidi kuliko zilizopita, kwani timu zote zina wachezaji wapya kabisa waliosajiliwa kwa ajili ya msimu huu, na baadhi watakuwa wakicheza 'dabi' hiyo kwa mara ya kwanza.

Wachezaji wapya kwa Simba ambao huenda wakawa uwanjani leo ni pamoja na Pape Sakho, Sadio Kanoute, Peter Banda, Henoc Inonga, Duncan Nyoni, Kibu Denis na Israel Mwenda huku Fiston Mayele, Djuma Shaaban, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Yusuph Athumani, Khalid Aucho na Djigui Diara kwa Yanga wakicheza dabi hiyo kwa mara ya kwanza.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Julai 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma ambapo Simba ilishinda bao 1-0, shukrani kwa beki Mganda, Thadeo Lwanga, lakini leo watani hao watakuwa wanakutana kwa mara ya tatu mwaka huu.

Iwapo Yanga itashinda leo itaifikia Simba kwa idadi ya kutwaa ngao hiyo, kwani takwimu zinaonyesha wameshinda mara tano, huku Wekundu wa Msimbazi wakitwaa mara sita.

Kuelekea mchezo wa leo, Kocha Mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi amesema anafurahi kuwa miongoni mwa makocha watakaosimama katika mchezo huo ambao kwake ni mara ya tatu tangu alipotua hapa nchini.

Nabi alisema mechi hiyo ni muhimu sana kwake kwa sababu si tu 'dabi', bali ni fainali ambayo anatafuta bingwa atakayeanza msimu na taji mkononi.

"Siwezi kuahidi ushindi kwenye mchezo huo, nafanya kazi yangu ili kupata matokeo mazuri, tumeondolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inatulazimu kupambana kushinda mechi hii ili kuwapa furaha mashabiki na viongozi. Hakutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwa sababu kuna changamoto kubwa ya kutumia wachezaji wa kigeni nane kati ya 12 tuliowasajili, " Nabi alisema.

Aliongeza wamejiandaa kupambana kuhakikisha wanapata ushindi ana imani na wachezaji wake licha ya bado hawajaungana na kutengeneza kombinesheni nzuri anayohitaji.

"Mashabiki watarajie kupata matokeo mazuri, nawapenda sana Wana-Yanga, wanipe muda na waniamini kwa sababu timu yangu inahitaji muda na kuwa bora zaidi ya ilivyo sasa," aliongeza kocha huyo.

Didier Gomes, Kocha Mkuu wa Simba alisema timu yake inauchukulia 'uzito' mkubwa mchezo wa leo kwa sababu wanahitaji ushindi na si pointi.

"Tutaingia na hesabu zetu, tutaingia tofauti na ambavyo wamewahi kutuona, ni mechi ninayohitaji matokeo, si mchezo wa kuangalia au kujaribu mtu," Gomes alisema.

Yanga itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kukosa taji lolote msimu uliopita wakati Simba ilitetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA.

Waamuzi wa mchezo huo wa watani wa jadi ni Ramadhani Kayoko atakayesaidiana na Frank Komba, Sudi Lila na Elly Sasii atakuwa mezani wakati Kamisaa ni Sarah Chao kutoka Manyara.

Katika kuhakikisha kila timu inapata ushindi, vikao vya viongozi na wanachama wa klabu hizo mbili vimeendelea kufanyika sehemu mbalimbali hapa nchini.

Baada ya mechi ya leo, Simba itaelekea Musoma kuwafuata wenyeji wao Biashara United wakati Yanga yenyewe itakwenda kwenye Uwanja wa Kaitaba kuwakabili Kagera Sugar.