Watanzania wahimizwa matumizi nishati mbadala

11Aug 2020
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Watanzania wahimizwa matumizi nishati mbadala

WATANZANIA wametakiwa kutumia nishati mbadala ili kusaidai taifa kuondokana na janga la uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya nishati ya mkaa, hali inayochangia mabadiliko ya tabia nchi.

Hayo yalibainishwa juzi jijini Dodoma na Meneja Masoko wa Kampuni ya Premium Active Tanzania Ltd, inayozalisha nishati mbadala ya mkaa mweupe Aristotle Nikitas, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Nikitas, alisema matumizi ya mkaa mweusi ambao unatumika hivi sasa katika maeneo mengi ya nchi umekuwa ndiyo chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira.

Alisema, umefika wakati sasa Watanzania wakabadili mitazamo yao na kuanza kutumia nishati mbadala ambazo hazina madhara kwa afya zao pamoja na mazingira.

“Huu mkaa mweupe ambao leo tunautangaza hapa Dodoma ni nishati ambayo ni rafiki wa mazingira kwa kuwa tunatengeneza kwa kutumia majani maalumu ambayo tunayapanda wenyewe na wala hatuharibu mazingira kabisa,” alisema Nikitas.

Alisema, mkaa unaotumika hivi sasa umeharibu uoto wa asili kwa kiasi kikubwa na kusababisha kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabia nchi.

“Mkaa mweupe huu ni rafiki wa mazingira, lakini afya ya watumiaji kwani mkaa ule mweusi pamoja na kuharibu mazingira, pia umekuwa si rafiki kwa afya ya watumiaji una hewa ya carbon kwa asilimia 80, hii ni hatari sana kwa afya,” alisema.

Kadhalika, alisema mkaa mweupe ni salama kwa afya ya mtumiaji kwa kuwa una kiasi cha asilimia tisa ya hewa ya carbon hivyo ni salama zaidi.

“Hivi sasa tumekuwa tukitoa elimu katika shule na maeneo mbalimbali juu ya matumizi ya mkaa huu mweupe ili jamii iondokane na matumizi ya mkaa mweusi ambao si salama kwa afya zao pamoja mazingira,” alisema.

Vilevile, alisema kutokana na wafanyabiashara ya mkaa kuangalia maslahi yao binafasi wanakata kila mti bila kujali aina ya sumu zilizomo kwenye mti husika.

“Kila mti hua una sumu yake, hivyo wafanyabiashara hawana muda wa kuangalia mti gani wa kukata, wanakata kila mti hivyo watumiaji ndio wanaweza kuwa katika hatari ya kupata madhara mbalimbali ya kiafya,” alisema.

Habari Kubwa