Yanga kujadili Ligi Kuu, FA Cup

07Apr 2020
Saada Akida
Nipashe
Yanga kujadili Ligi Kuu, FA Cup

LICHA ya kutojulikana kwa hatma ya Ligi Kuu Bara kuendelea au kufutwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga, Hamad Islam, amesema wako katika mipango ya kukutana na wajumbe wenzake ili kujadili mwenendo wa timu yao kuelekea michezo iliyobaki na Kombe la Shirikisho la Soka nchini.

Akizungumza na Nipashe jijini jana, Islam alisema wanampango wa kukutana na wajumbe wote wa kamati hiyo kwa ajili ya kujadili mwenendo wa timu yao ikiwamo malengo yaliyopo katika michuano ya FA na kuhakikisha timu yao inafanya vizuri kumaliza nafasi ya pili.

Alisema wajumbe wa kamati husika watahakikisha naweka mikakati ya michezo iliyobaki huku wakiipa kipaumbele michuano ya FA ambayo bingwa huiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kwa sasa kuna janga hili la virusi vya corona, tuombe Mungu limalizike maana kuna mambo mengi ya kimaendeleo yamesimama, pia tuna mpango wa kukutana na wajumbe kujadiliana mambo mengi,” alisema Islam.

Alisema kwa sasa wapo makini kuweka mambo sawa kuhakikisha kikosi chao kinafanya vizuri katika michezo hiyo kwa kumaliza ligi katika nafasi ya pili na kutwaa taji la FA ambalo litawapeleka katika michuano ya kimataifa.

Aidha, kuhusu usajili, alisema hawataingilia majukumu ya benchi hilo la ufundi, linaloongozwa na kocha Mbelgiji Luc Eymael, kwa aina ya wachezaji ambao amewapendekeza katika ripoti aliyoiacha.