Yanga SC yazindua Twenzetu Mabadiliko

20May 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yanga SC yazindua Twenzetu Mabadiliko

MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Msolla, amezindua kampeni ya kuelekea uzinduzi wa mfumo wa mabadiliko ya kiundeshaji kwa klabu hiyo kongwe nchini.

MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Msolla:PICHA NA MTANDAO

Akizungumza kwenye mtandao rasmi wa klabu hiyo jana, Dk. Msolla alisema kamati hiyo ya mabadiliko itakuwa chini ya kamati ndogo itakayosimamiwa na Mwanasheria Msomi Alex Mgongolwa huku mchakato wote wa mabadiliko ya kimfumo ukisimamiwa na kufadhiliwa na mdhamini mkuu GSM ukiwa na kauli mbiu 'Twenzetu Kwenye Mabadiliko'.

Dk. Msolla alisema huu ni mwanzo halisi wa kuelekea kuweka sahihi makubaliano hayo ambayo ndiyo itakuwa muda rasmi wa mchakato huo wa mabadiliko kuanza.

"Moja ya dhamira yangu wakati nagombea uongozi ilikuwa ni kubadilisha muundo wa uendeshaji, sasa nadhani ndoto hii inaelekea kukamilika. Ombi langu kwa wanachama wa Yanga tuwe kitu kimoja, tuungane na viongozi tuungane na wadhamini ili tuweze kufanikisha hilo," alisema Dk. Msolla.

Yanga inataka kubadilika kuwafuata watani zao wa jadi Simba ambao tayari wameshaenda kwenye mfumo mpya wa uendeshaji.