Yikpe nje ripoti Eymael Yanga

07Apr 2020
Saada Akida
Nipashe
Yikpe nje ripoti Eymael Yanga

Huku Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael akiwa tayari amekabidhi ripoti yake ya wachezaji anaotaka wasajiliwe na wale wa kutemwa kuelekea msimu ujao, jina la mshambuliaji Muivory Coast Gnamien Yikpe, ni miongoni mwa wachezaji ambao hawatakuwapo katika kikosi chake, imefahamika.

Taarifa za uhakika zilizolifikia Nipashe jijini jana kutoka kwa kiongozi mmoja wa ngazi za juu ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, zilieleza wanalazimika kumjadili mshambuliaji huyo kuwamo katika orodha ya kutemwa kutokana na kushindwa kufanya walichokitarajia.

Alisema nafasi ya kubaki ni ngumu sana katika kikosi cha timu yao kutokana na nyota huyo kushindwa kufikia malengo yao licha ya kupewa nafasi ya kucheza katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu.

“Yikpe hana nafasi kwa msimu ujao, kwani ukiangalia ripoti iliyoachwa na Luc ni ya kuhitaji washambuliaji wawili, hii inaonyesha kwamba mchezaji huyo hana nafasi ya kuendelea kutumikia kikosi hiki,” alisema kiongozi huyo.

Wakati huo huo Kocha Msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwassa, alisema hatma ya nyota huyo litajadiliwa na jopo zima la benchi la ufundi likiongozwa na Luc pamoja na kamati ya usajili na ufundi.

“Yikpe ameshindwa kwenda na mazingira hadi kushindwa kufikia malengo yaliyotarajiwa, kwani alivyokuja mwanzoni alifanya vizuri, lakini amebadilika ghafla, amekuwa akifanya vizuri mazoezi, lakini katika mechi ni tofauti na kile ambacho anaambiwa,” alisema Mkwasa.

Alisema mpira ni mchezo wa kupanda na kushuka, benchi lilijitahidi kumpa nafasi katika baadhi ya michezo ya ligi, lakini akawa anafanya mambo tofauti na kile kinachotarajiwa kabla ya kusajiliwa.