Yondani, Abdul waziingiza vitani Gwambina, Namungo

11Aug 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Yondani, Abdul waziingiza vitani Gwambina, Namungo

WAKATI klabu ya Namungo ikisema kuwa itasajili wachezaji wanane kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na mechi za kimataifa, wachezaji wawili walioachwa na Yanga, Kelvin Yondani na Juma Abdul huenda wakajiunga na timu hiyo licha ya kuhusishwa Gwambina FC iliyopanda daraja msimu huu.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Zidadu, amesema wanatarajia kusajili wachezaji nane kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika (Caf) wenye uwezo wa kuwasaidia kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.

"Tumeshaanza mchakato wa usajili kwa wachezaji wapya ili kuongeza nguvu kikosini, lakini tunawaongezea mikataba wachezaji wa zamani ambao muda wao wa mikataba umemalizika, lengo ni kufanya vema kwenye michuano ya Ligi Kuu na kimataifa kwa sababu ikumbukwe kuwa tunawakilisha nchi, hivyo usajili ni lazima uwe wa kimataifa kwa wachezaji wa nje na wa ndani wawe wazuri na wazoefu, kwa hiyo mashabiki wetu watulie, wasihofu kuhusu usajili," alisema mwenyekiti huyo.

Ingawa hakutaja ni wachezaji gani ambao imeanza mchakato wa kuwasajili, lakini habari za ndani zinaeleza kuwa klabu hiyo iko kwenye mazungumzo na Yondani na Abdul ambao hivi karibuni waliachwa na klabu ya Yanga baada ya kutoafikiana kwenye mchakato wa kuongeza mkataba.

Inadaiwa kuwa lengo la Namungo kutaka kusajili wachezaji hao haswa ni kutokana na kuwa na uzoefu kwenye mechi za kimataifa ambazo inakwenda kucheza, huku wachezaji wake wengi wakiwa hawana uzoefu huo.

Namungo ambayo imeanza kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu, itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ratiba yake itatolewa baadaye mwaka huu.

Hata hivyo, zipo taarifa kuwa wachezaji hao pia wanawaniwa na Gwambina FC ambao nao wameonyesha nia ya kuwasajili na mazungumzo kati ya pande mbili yanaendelea.

Habari Kubwa